Changamoto ya upotevu wa mazao ya uvuvi yaanza kupatiwa majibu

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega akizungumza na wanakijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya
ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha
kuzalisha barafu kilichojengwa na
Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa
ufadhili wa Climateworks Foundation na kuipongeza WWF kwa kuyafanyia
kazi maono ya serikali ya kuhifadhi mazao ya uvuvi ambayo yamekuwa
yakiharibika kutokana na kukosekana kwa nyenzo za kuyahifadhi ikiwemo
barafu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akipeana mkono na Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa Tanzania,
Dkt. Amani Ngusaru mara baada ya Dkt. Ngusaru kuzungumzia mradi wa
miaka miwili wa WWF katika kijiji cha Songosongo kilichopo Wilaya ya
Kilwa Mkoani Lindi, uliowezesha kupatikana Tani 91,000 za samaki aina ya
pweza zenye thamani ya Shilingi Milioni 458, wakati wa hafla fupi ya
kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kijijini hapo.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti
wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei akizungumza na
wanakijiji cha Songosongo (hawapo pichani) kilichopo Wilaya ya Kilwa
Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo cha kuzalisha
barafu kilichojengwa na
Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa
ufadhili wa Climateworks Foundation na kuwaasa wanakijiji hao
kuhakikisha uvunaji wa samaki aina ya pweza unakuwa endelevu na kutumia
vyema kituo hicho ili kiwe na tija katika kuzuia upotevu wa mazao ya
uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto) akimshuhudia Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa Tanzania,
Dkt. Amani Ngusaru na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya na Kijiji cha
Songosongo katika utiaji saini wa makabidhiano ya kituo cha kuzalisha
barafu kilichopo Kijiji cha Songosongo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi,
wakati wa hafla fupi ya kukabidhi kituo hicho.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega akiwasha moja ya mitambo ya kuzalisha barafu ikiwa ni
ishara ya kuanza rasmi kutumika kwa kituo cha kuzalisha barafu
kilichojengwa na
Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa
ufadhili wa Climateworks Foundation katika Kijiji cha Songosongo
kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya
kukabidhi kituo hicho.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Abdallah Ulega akiangalia ubora wa barafu iliyozalishwa na moja ya
mitambo iliyopo kwenye kituo cha kuzalisha barafu katika kijiji cha
Songosongo kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi. Kushoto kwake ni
Mkurugenzi Mkazi wa
Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) Dkt. Amani Ngusaru ambapo kituo hicho kimejengwa na WWF kwa ufadhili wa Climateworks Foundation.

Muonekano wa kituo cha kuzalisha barafu kilichopo Kijiji cha Songosongo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, kilichojengwa na Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kwa
ufadhili wa Climateworks Foundation kwa thamani ya Shilingi Milioni 424
na kina uwezo wa kuzalisha barafu Tani 1.4 kwa saa 24.

………………………………………………………………………………….

Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ameupongeza Mfuko wa Uhifadhi wa
Mazingira Duniani (WWF), kwa kuyafanyia kazi maono ya serikali ya
kuhifadhi mazao ya uvuvi ambayo yamekuwa yakiharibika kutokana na
kukosekana kwa nyenzo za kuyahifadhi.
Naibu Waziri Ulega
amebainisha hayo (01.05.2021) akiwa katika Kijiji cha Songosongo
kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, wakati wa hafla fupi ya
kukabidhi kituo cha kuzalisha barafu kilichojengwa na WWF kwa ufadhili
wa Climateworks Foundation chenye thamani ya Shilingi Milioni 424, kwa
ajili ya kuhifadhia samaki wanaovuliwa na wanakijiji hao.
Amesema Wizara ya Mifugo
na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2021/22 imeweka mipango mbalimbali ya
kuhakikisha inaongeza vituo vya kuhifadhia mazao ya uvuvi ili wavuvi
waondokane na changamoto ya samaki kuharibika kutokana na ukosefu wa
barafu na maeneo ya kuyahifadhia mazao hayo.
“Hali duni inachangiwa na
upotevu wa mazao wanayovua kutokana na uvuvi na pia kutokuwa na uhakika
wa masoko ya mazao wanayoyapata ndiyo maana serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan inakuja na suluhu kuokoa
wavuvi na watanzania kwa ujumla wake.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha, katika kuhakikisha
mazao ya uvuvi yanakuwa na masoko ya uhakika Mhe. Ulega amesema azma ya
wizara hiyo ni kuona mazao hayo yanasimamiwa na ushirika hali ambayo
itasaidia kuwa na umoja ambao utawezesha wavuvi kusikilizwa na kupata
masoko kwa pamoja.
Pia, amesema Wizara ya
Mifugo na Uvuvi itakuja na mkakati wa usambazaji na uhamasishaji wa
matumizi ya vichanja maalum kwa ajili ya kukaushia dagaa na samaki ili
kuzuia mazao hayo kutokuwa na mchanga na kuyaongezea thamani kwa kupata
masoko zaidi ndani na nje ya nchi hali itakayobadilisha uchumi wa wavuvi
na serikali kupata mapato zaidi.
Kuhusu zao la mwani
ambalo wanakijiji cha Songosongo wamelalamikia kukosa masoko hali
inayosababisha nyumba zao kurundikana zao hilo na hatimaye kuharibika na
wakati mwingine kuuza kwa bei ndogo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdallah Ulega amesema katika kipindi hiki wizara itapitia upya
sheria inayosimamia zao la mwani ili kubaini changamoto ambazo ni kero
kwa wafanyabiashara wa zao hilo na kuziondoa ili wakulima wa mwani na
wafanyabiashara waweze kunufaika.
“Moja ya jambo ambalo
pamoja na kutafuta soko la mwani tutengeneze kiwanda kidogo cha kukausha
mwani na kuliongezea thamani zao hilo ili wakulima waweze kuhifadhi
vizuri mwani na kuuza kwa bei nzuri zaidi kuelekea katika uchumi wa
bluu.” Amefafanua Mhe. Ulega
Ameongeza kuwa kupitia
zao la mwani wanakijiji cha Songosongo wataweza kutengeneza bidhaa
mbalimbali zitokanazo na mwani ikiwemo sabuni na kuuomba Mfuko wa
Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kufikisha elimu ya ujasiriamali kwa
wanakijiji hao juu ya masuala ya ujasiriamali.
Naibu Waziri Ulega pia
amesema ni wakati muafaka kwa serikali kuangalia upya Vikundi vya
Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) badala ya kulinda rasilimali za
uvuvi pekee viweze kunufaika kwa kupata mikopo na kuendesha shughuli
zao.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkazi wa WWF Tanzania Dkt. Amani Ngusaru amesema kituo cha
kuzalisha barafu kilichojengwa katika Kijiji cha Songosongo Wilaya ya
Kilwa Mkoani Lindi chini ya ufadhili wa Climateworks Foundation chenye
thamani ya Shilingi Milioni 424, kina uwezo wa kuzalisha barafu Tani 1.4
kwa saa 24.
Dkt. Ngusaru amesema
mradi huo umeenda sambamba na uhamasishaji wa ufungaji wa miamba ya
samaki aina ya pweza ambapo inakadiriwa kwa kipindi cha miaka mwili ya
mradi, Tani 91,000 za pweza zimevuliwa katika Kijiji cha Songosongo
zenye thamani ya Shilingi Milioni 458, ambapo fedha hizo zimetokana na
ufungaji wa miamba kwa awamu tano.
Ameongeza kuwa kuhusu
changamoto za zao la mwani anaanza kulifanyia kazi kwa kuwasiliana na
makao makuu ya WWF ili kupata namna bora ya wakulima wa zao la mwani
hapa nchini wakiwemo wa Kijiji cha Songosongo kuwa na masoko ya uhakika
ya zao hilo.
Aidha, kuhusu kilio cha
kukosekana kwa boti ya doria kwa ajili kikundi cha BMU katika Kijiji cha
Songosongo, Dkt. Ngusaru amesema WWF imepokea kilio hicho na kuahidi
kuleta boti na injini yake ili kurahisisha shughuli za doria katika
maeneo ya miamba ya uzalishaji wa samaki aina ya Pweza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Utafiti Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ishmael Kimirei amesema ili
kuhakikisha kituo cha uzalishaji barafu kilichopo katika Kijiji cha
Songosongo kinakuwa na tija ni lazima uvuaji wa samaki aina ya pweza uwe
endelevu na kuhakikisha upotevu wa samaki hao unapunguzwa kwa kiasi
kikubwa.
Dkt. Kimirei ametolea
mfano wa moja ya mitambo ya uzalishaji barafu iliyowekwa katika mwambao
wa Ziwa Tanganyika lakini wavuvi wakafikiri barafu zinaharibu samaki na
hawakutaka kuutumia, lakini wavuvi hao walipokuja kugundua faida ya
barafu hivi sasa mahitaji ya barafu hayatoshi.
Amefafanua kuwa mitambo
hiyo ni muhimu na imetumia fedha nyingi hivyo wanakijiji cha Songosongo
waweze kutumia kwa namna ambavyo imepangwa kutumiwa na kuitunza mitambo
hiyo kwa ajili ya uhifadhi wa samaki aina ya pweza pamoja na samaki
wengine.
Nao baadhi ya wanakijiji
cha Songosongo wamesema wamefurahishwa na kuwepo kwa kituo hicho cha
kuzalisha barafu hali ambayo itawasaidia kuzalisha barafu kwa wingi na
kutunza samaki ili wasiharibike na kuiomba serikali pamoja na WWF
kuangalia namna ya kuwasaidia waweze kunufaika na zao la mwani kwa kuwa
kwa sasa wafanyabiashara wengi wanashindwa kwenda kununua kutokana na
gharama za ushuru hali inayosababisha wakulima wa zao hilo kufikia kuuza
Kilogramu Moja ya mwani kwa Shilingi 400.