DC Kaganda ataka Madiwani kuacha migongano

Egidia Vedasto
Arusha.

Madiwani wa Halmashauri ya Arusha DC wametakiwa kushirikiana katika utendaji kazi wao na kuacha migongano isiyo ya lazima ili kujenga imani kwa wananchi juu ya Serikali ya awamu ya sita.

Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Arusha, DC Emmanuela Kaganda, amewahimiza kuzingatia viapo vya maadili vinavyowataka kutumikia wananchi kwa hali na mali bila upendeleo na ubaguzi ili kuinua uchumi wao na Taifa kama inavyotakiwa.

Aidha Kaganda amelihakikishia Baraza kuwa ofisi yake itaendelea kupambana na changamoto ambazo zimeendelea kuwa gumzo ikiwemo suala la Mafuriko, Ujenzi wa Kituo cha polisi Moivo, kusogeza Ofisi za NIDA karibu na wakazi, ulinzi na usimamizi wa mlima Kivesi, na kuwataka Madiwani wote kutoa ushirikiano wa kina ili kufanikisha malengo hayo.

“Msisahau kwamba mnaaminiwa na wananchi kwa sababu wanawafahamu, sasa mkitenda kazi chini ya kiwango, msipoeleza miradi inayotekelezwa katika kata zenu, msipo taja fedha mnazopata kutekeleza miradi na kusimamia watendaji kuzuia ubadhilifu wa fedha, msipowahimiza Watendaji kuwasomea wananchi mapato na matumizi mtaaminikaje katika uchaguzi ujao mwakani? “Kaganda amehoji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arusha DC Ojung SaleKwa amesema watazingatia maagizo na ushauri uliotolewa na DC Kaganda ili kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati.

Pia ametolea ufafanuzi taarifa zilizokuwepo hapo awali za upotevu wa fedha zaidi ya shilingi milioni 600, kwamba kiasi hicho hakikuwa cha kweli badala yake ilikuwa shilingi milioni 499 na fedha hizo zote tayari zimerudishwa katika vituo vya afya na zahanati kwa lengo la kukamilisha miradi.

“Fedha hizo zilipotelea katika baadhi ya taasisi na kuwahusisha baadhi ya watumishi wasio kuwa waadilifu, tayari wamechukuliwa hatua kali na pesa zote zimerudi” Amesema Salekwa.

Mmoja wa Madiwani Eliakim Marivey wa Kata ya Kimnyak ameipongeza Serikali kwa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kata yake ikiwemo ya afya na elimu.

“Changamoto kubwa inayonipa hofu hasa katika kipindi hiki tunapoelekea mvua za vuli ni mafuriko katika kata yangu ambayo yamekuwa changamoto kwa wananchi muda mrefu, lakini kwa kuwa Mheshimiwa DC ameahidi kutukutanisha na Wadau husika TANROADS na TARURA naamini hali itakuwa shwari” ameeleza Marivey.

Sambamba na hayo Afisa Maadili Kanda ya Kaskazini Tumaini Mgalla amewakumbusha Madiwani na Wakuu wengine wa Idara yawapasayo kuzingatia kuwa ni pamoja na kuepuka tamaa, matumizi mabaya ya mali za umma kama magari na pesa zinazotokana na kodi za wananchi, kutoa huduma kwa upendeleo, ukabila au udini, na kila mmoja awajibike ili kusonga mbele na kuepuka makundi.

“Wakuu wa Idara na Madiwani mlioko hapa msisahau kiapo cha maadili na hati ya maadili mliyopewa, kumbuka mlivyoahidi ili kuepuka migongano, utakapokiuka kiapo hicho utaonywa, kushushwa cheo au kuvuliwa madaraka” amefafanua Mgalla.

Viongozi mbalimbali katika Baraza la Madiwani Arusha DC kushoto ni Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais Sekretariet ya Maadili Kanda ya Kaskazini Gerald Mwaitebele