NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amekabidhi mifuko 100 ya saruji ili kushiriki ujenzi wa Msikiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, kwa niaba ya Dk. Bashiru alikabidhi saruji hiyo jana kwa Kaimu Sheikhe wa Mkoa Alhaji Sheikhe Hassani Kabeke.
Kwa mujibu wa Mongela, saruji hiyo ni ahadi ya Katibu Mkuu huyo wa CCM aliyoitoa mapema Agosti mwaka huu, alipotembelea na kuzungumza na viongozi wa taasisi mbalimbali za dini mkoani Mwanza.
Akiwa kwenye ofisi za BAKWATA zilizopo Mbungani katika Wilaya ya Nyaagana, Dk. Bashiru alikuta uongozi wa taasisi hiyo chini ya kaimu Sheikhe wa Mkoa, alhaji Kabeke ukiwa kwenye mchakato wa ujenzi wa msikiti wa baraza hilo na kuahidi kushiriki kwa kutoa mifuko 100 ya saruji.
Akipokea saruji hiyo, Sheikhe Kabeke alimshukuru Dk. Bashiru kwa kutekeleza ahadi yake kwa sababu siku ya kiama wote walioahidi watahojiwa.
Alisema serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli ni ya ahadi na vitendo kutokana na kutekeleza ahadi zake kwa wananchi ukweli uliodhihirishwa pia na Dk. Bashiru.
“Siku ya kiama ahadi zote wale waliaohidi wataulizwa lakini kwa kitendo hiki cha Katibu Mkuu kutimiza ahadi yake ni ishara njema kwa sababu tunaona serikali imetekeleza ahadi zake nyingi.Tunaamini mambo mengi yamefanyika na ahadi zitaendelea kutekelezwa na serikali yetu,”alisema.
Sheikhe Kabeke alisema kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu, waislamu wajitokeze na kuwa mstari wa mbele siku hiyo ili kupiga kura kuchagua viongozi waadilifu, wazalendo na wenye uwezo wa kuleta maendeleo kwa jamii na kuyasimamia.