Dkt. abbasi: serikali imeweka mifumo ya kisheria na kitaasisi kwa maendeleo endelevu ya watanzania

Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
SERIKALI
imesema imeweka mifumo imara ya kitaasisi na kisheria inayohakikiwa
kuwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na itakayotekelezwa na Serikali
ya Awamu ya Tano inaendelea kuleta manufaa endelevu kwa faida ya
Watanzania wote.

Hayo
yamebainishwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya
Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi wakati
wa mkutano wake na Waandishi wa Vyombo vya Habari aliozungumzia
kuhusiana na tathimini ya miaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt. John
Magufuli.

Dkt.
Abbasi alisema yapo mambo mengi na miradi mikubwa ya maendeleo
inayotekelezwa na itakayotekelezwa na Serikali ya Awamu hivyo ili
kuwezesha mafanikio yake yanaleta matokeo chanya kwa Watanzania na jamii
kwa ujumla, Serikali imeweka mifumo imara ya kitaasisi na kisheria kwa
ajili ya kulinda mafanikio hayo hata baada ya Serikali ya Awamu ya Tano
kumaliza muda wake.

‘‘Tanzania
kwa sasa ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne ya Utawala wa Serikali
ya Awamu ya Tano tumeweza kufanya mambo mengi ikiwemo suala la rushwa
ambalo limekuwa kero kubwa kwa Watanzania na hilo kwa sasa tumeunda
Mahakama maalum ya Mafisadi ambayo tayari imesikiliza  kesi zaidi ya
50’’ alisema Dkt. Abbasi.

Aidha
aliongeza zipo ahadi za utelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ya
Serikali iliyoahidiwa kufanywa na Rais Dkt. John Magufuli ambayo awali
ilikuwa ikileta kero na kuchelewesha maendeleo ya Watanzania, ambapo
ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne ya utawala wa Serikali ya Awamu
ya Tano yameweza kutekelezwa.

Akifafanua
zaidi Dkt. Abbasi alisema ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi
wa Rais Dkt. John Magufuli, Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kutimiza
ahadi mbalimbali ambazo tayari zimeanza kuleta matokeo chanya kwa
Watanzania ikiwemo ununuzi wa ndege za Serikali ambapo awali jambo hilo
lilikuwa na ugumu katika utekezaji wake.

‘Jambo
jingine ni suala la kuhamia Dodoma, jambo hili kwa sasa si ndoto tena
kwani kwa sasa asilimia 90 ya watumishi wa Serikali katika Wizara na
baadhi ya Idara, Taasisi na Wakala za Serikali wamehamia Dodoma na
Serikali imeweza msingi wa kisheria wa kuitangaza Dodoma kuwa ni makao
makuu ya Serikali’’ alisema Dkt. Abbasi.

Kwa
mujibu wa Dkt. Abbasi alisema ili maendeleo hayo yazidi kuleta manufaa
endelevu kwa vizazi vijavyo, Watanzania hawana budi kuwa wazalendo na
kuwa walinzi wa mali za umma na kutoa taarifa katika mamlaka za serikali
kuhusu uharibifu na ubadhirifu unaofanywa na mtu au kikundi chochote
katika jamii.

Kwa
mujibu wa Dkt. Abbasi alisema Serikali ya Awamu ya Tano kupitia
ushirikiano wake na wananchi imeweza kutekeleza miradi mikubwa ya
maendeleo ya kijamii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, maji,
elimu na barabara, ambayo imeendelea kuwagusa wananchi wengi zaidi
hususani wa kipato cha chini.

Akitolea
mfano, Dkt. Abbasi alisema Serikali inatekeleza miradi ya maji 1600
nchi nzima ikiwemo miradi 300 inayotekelezwa katika maeneo ya vijijini
na kutumia kiasi cha Tsh Bilioni 700 kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo
katika maeneo ya mijini ili kuhakikisha kuwa inafikia kiwango cha
asilimia 85 vijijini na asilimia 95 maeneo ya mijini ifikapo mwaka 2020.

Kuhusu
sekta ya afya, Dkt. Abbasi alisema Serikali kwa sasa imeendelea
kuimarisha sekta hiyo kwani kwa sasa Tanzania imekuwa nchi mfadhili kwa
kuweza kufanya huduma mbalimbali za kibingwa ambazo zilikuwa zikifanyika
nje ya nchi na kuifanya Serikali kupoteza kiasi kikubwa cha fedha za
Watanzania.

‘Ndani
ya kipindi cha miaka minne Serikali imeweza kuongeza bajeti ya dawa na
vifaa tiba kutoka Tsh Bilioni 31 mwaka 2014/15 hadi kufikia Bilioni 270,
na pia kuajiri waganga wataalamu zaidi ya 6000 wanaohudumia wagonjwa
katika hospitali zetu za Mikoa, Wilaya, Vituo vya Afya katika Kata na
Zahanati katika maeneo ya vijijini’’ alisema Dkt. Abbasi.