Hatuwaadhibu walimu ili kuwakomoa bali kuwajenga kimaadili – chitama

 

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania, Moses Chitama.

Veronica Simba – TSC

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa
Walimu Tanzania (TSC), Moses Chitama ameitaka jamii kuelewa kwamba
adhabu zinazotolewa kwa walimu wanaobainika kwenda kinyume na maadili
hazilengi kuwakomoa bali zipo kisheria ili kuhakikisha nidhamu na
maadili ya kada hiyo yanazingatiwa.

Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti hivi
karibuni wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari nchini
kuhusu nidhamu na maadili kwa walimu nchini.

Chitama alieleza kuwa, ualimu ni taaluma
kama zilivyo taaluma nyingine hivyo ina miiko, taratibu na sheria zake
zinazoiongoza na zinapokiukwa, Tume inawajibika kuchukua hatua ili
kuhakikisha shule zinabaki kuwa mahala salama na sahihi kwa watoto
wanaohusika.

“Ndiyo maana walimu hufundishwa tangu
wakiwa vyuoni namna bora ya kuwalea watoto watakaokwenda kuwafundisha
ili wawe raia wema katika jamii na Taifa kwa ujumla.”

Akizungumzia ukiukwaji wa maadili
unaofanywa na baadhi ya walimu, Chitama alikiri kuwa tatizo hilo lipo na
kuongeza kuwa changamoto ambayo imekithiri kwa sasa ni baadhi ya walimu
kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.

Alisema, Tume ya Utumishi wa Walimu,
ambayo ni Mamlaka ya Nidhamu, imekuwa ikilikemea sana suala hilo na
imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kulitatua ikiwemo
kutoa semina za kuwajengea uelewa walimu na kwa wanaothibitika kutenda
kosa hilo, hupewa adhabu ya kufukuzwa kazi.

Aidha, alitaja changamoto nyingine kuwa
ni utoro kazini kwa baadhi ya walimu ambapo alibainisha kuwa uchunguzi
uliofanywa na Tume umebaini kuwa baadhi ya wanaotoroka huenda kufanya
kazi katika shule za binafsi huku wakiendelea kupokea mshahara wa
serikali.

“Sasa kweli kwa hali kama hiyo ambapo
wanafunzi wanakoseshwa haki yao ya msingi ya masomo na wengine
kunyanyaswa kijinsia, unatarajia Tume ikae kimya tu? Ni lazima tuchukue
hatua stahiki ili kukomesha hali hiyo,” alisisitiza Chitama.

Kwa upande mwingine, Kaimu Katibu huyo
amewaasa wazazi kutimiza wajibu wao kwa kushirikiana na walimu katika
malezi ya watoto badala ya kuwaachia walimu peke yao jukumu hilo.

Akifafanua, alisema baadhi ya wazazi
wamekuwa wakikwepa kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto kwa
kisingizio cha kukosa muda kutokana na kazi wanazozifanya kujipatia
kipato, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili kwa
watoto.

Tume ya Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya
Ajira na Nidhamu kwa walimu wa shule za msingi na sekondari walio kwenye
utumishi wa umma, Tanzania Bara.

Imeundwa kwa Sheria Namba 25 ya mwaka
2015 na ilianza kufanya kazi rasmi mwaka 2016 baada ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kupitisha sharia na kanuni zake.