Jamii yaombwa kuwashika mkono watoto yatima

Na Amiri kilagalila-Njombe
Jamii
nchini inaombwa kuendelea kutoa mchango katika vituo vya kulea watoto
yatima pamoja na kusaidia watoto katika malezi,ili kuendelea kupunguza
changamoto zinazovikabili vituo vya kulea watoto nchini.


Ombi
limetolewa na baadhi ya walezi wa vituo vya kulea watoto yatima Njombe
mjini mara baada ya hafla ya chakula cha mchana baina ya vituo vya kulea
watoto mjini humo pamoja na viongozi wa ustawi wa jamii na maendeleo ya
jamii wa mji wa Njombe iliyofanyika katika kituo cha kulea watoto
yatima cha St.Anne kilichopo Uwemba mjini humo.

Sista
Maria Mgeni ni msimamizi wa shule ya watoto yatima mtakatifu Donbosco
iliyopo Unewa kijiji cha Madobole kata ya Luponde,anasema licha ya
serikali na baadhi ya wahisani kutoa michango ya hali na mali ili
kuendeleza vituo hivyo lakini bado wanaiomba jamii kuendelea kujitoa kwa
kuwa bado changamoto zinaendelea kukabili vituo.

“Ningeomba
msaada jamii iendelea kuchangia chochote iwe mavazi,chakula,vitanda,
hata Magodoro na kwa upande wa serikali hasa maendeleo ya jamii na
ustawi wa jamii kwa kweli tunawashukuru sana kwa kuendelea kuwa pamoja
na sisi”Alisema Maria Mgeni

Naye
Sista Maria Mwinuka kutoka kituo cha kulea watoto yatima
St.Anne,amesema wameweza kupata mafanikio makubwa ikiwemo kuokoa maisha
ya watoto wengi wanaofika kituoni wakiwa na hali mbaya huku akiomba
jamii ijifunze kuwajibika katika kuwalea watoto.

“Wito
wetu jamii ijifunze kuwajibika kulea mtoto,katika familia za kiafrika
watoto hulelewa na jamii kwa hiyo mama akifariki,ndugu pande zote mbili
wahusike kumlea kwa karibu mtoto katika mazingira ya nyumbani”alisema
Sista Maria Mwinuka

Enembora
Lema ni afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya mji wa Njombe,amesema
serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na vituo kwa ajili ya
malezi ya watoto hivyo ametoa pongezi kwa kazi zinazofanywa na walezi.