Kanisa katoliki laishtumu serikali kuelekea uchaguzi mkuu 2020

media
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza

  
Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini
Burundi linasema linahofia ongezeko la visa vya ukiukwaji wa haki za
binadamu na wapinzani kusumbuliwa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka ujao,
wakati huu serikali nchini humo ikiwashtumu maaskofu hao kwa kuhubiri
chuki.

Jumapili
iliyopita, ujumbe wa maaskofu ulisomwa Makanisani kulalamikia ongezeko
la visa hivyo vinavyowalenga wapinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka
2020.

“Kumeendelea kushuhudiwa kwa visa vinavyowalenga wanasiasa wa upinzani, wenye maoni tofauti na serikali,”ujumbe huo ulieleza.
Shutuma
hizi zimekuja, baada ya mapema mwezi huu ripoti ya watalaam wa Umoja wa
Mataifa kumshtumu rais Pierre Nkurunziza kwa kuhusika binafsi katika
ukiukwaji wa visa hivyo.

Mwaka 2015, mzozo wa kisiasa ulisababisha
zaidi ya watu 1,000 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 400,000
kuyakimbia makwao baada ya rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania urais
kwa muhula wa tatu kinyume cha Katiba.

Mwaka 2018, kulikuwa na mabadiliko ya Katiba ambayo yatamwezesha rais Nkurunziza kuendelea kuwa madarakani hadi mwaka 2034.