Katibu mkuu tamisemi ataka sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 zifuatwe

Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi
Joseph Nyamhanga amewataka viongozi na wasimamizi wa Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Halmashauri
kuhakikisha kuwa wanasimamia kwa karibu Kanuni, Sheria, na Miongozo
mbalimbali iliyowekwa ili uchaguzi huo ufanyike katika mazingira ya
amani na uwe huru na haki.


Katibu
Mkuu ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akielezea hatua inayofuata
baada ya zoezi la uchukuaji na urejeshwaji wa fomu za kugombea nafasi
mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kukamilika hapo jana
ambapo amesema zoezi linaloendelea kwa tarehe 5 Novemba, 2019 ni Uteuzi
wa Wagombea katika nafasi za Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa na
nafasi ya Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji na Wajumbe wa Kamati za
Mitaa.

Amesema
kuwa kuanzia tarehe 5 hadi 6 Novemba, 2019 ni kipindi cha watu
walioomba kuteuliwa kuwa wagombea au wagombea wa nafasi mbalimbali za
uongozi ambao hawajaridhika na uteuzi uliofanywa na Wasimamizi Wasaidizi
wa Uchaguzi kuwasilisha pingamizi kuhusu uteuzi wa wagombea.

 “Nitoe
maelekezo kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kusimamia kwa weledi
zoezi la uwasilishaji wa pingamizi na kutoa uamuzi wa haki kuhusu
pingamizi hizo za uteuzi wa wagombea” amesisitiza Katibu mkuu.

Mhandisi
Nyamhanga ameseama kwamba baada ya Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi
kupokea pingamizi na kutoa uamuzi, waombaji au wagombea ambao
hawataridhika na uamuzi wa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi watakuwa na
haki ya kukata rufaa kati ya tarehe 5 hadi 8 Novemba,  2019 kwenye
Kamati za Rufani zilizoanzishwa katika kila Wilaya nchini.

Aidha,
Kamati za Rufani zitatoa uamuzi kuhusu rufaa mbalimbali
zilizowasilishwa kwake kati ya tarehe 5 na 9 Novemba, 2019.  Vilevile,
mtu yeyote ambaye ameomba kuteuliwa kuwa mgombea au mgombea ambaye
hajaridhika na uamuzi wa Kamati ya Rufani atakuwa na haki ya kufungua
kesi katika Mahakama ya Wilaya ndani ya muda wa siku 30 baada ya matokeo
ya uchaguzi kutangazwa.

Mhandisi
Nyamhanga amevikumbusha Vyama vya Siasa ambavyo vitashiriki katika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 kuhakikisha vinawasilisha
ratiba za mikutano ya kampeni kwa Wasimamizi wa Uchaguzi tarehe 10
Novemba, 2019 kama ilivyooneshwa kwenye ratiba ya Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa.