Mahakama yataka uthibitisho wa afya ya tundu lissu



Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema  wadhamini wa Mwanasheria Mkuu wa
CHADEMA, Tundu Lissu wanatakiwa kutoa uthibitisho wa maendeleo ya afya
ya Lissu pindi shauri hilo linapoitishwa tena mahakamani hapo.


Lissu
na wenzake watatu kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwemo
kuandika taarifa zenye maudhui ya uchochezi kinyume na Sheria ya
Magazeti ya Mwaka 2002.

Hayo
yamebainishwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kuuliza
maendeleo ya Lissu ndipo mdhamini wake, Robert Katula alidai kuwa
mshtakiwa huyo bado anaumwa.

Kutokana
na kauli hiyo, Wakili wa Serikali, Estazia Wilson ameieleza mahakama
kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa hivyo hawawezi kuendelea
na shauri hilo hivyo wataendelea kumsubiri Lissu hadi afya yake
itakapoimarika.

Hakimu
Simba alisema shauri hilo litakapokuja  mahakamani hapo mdhamini wa
Lissu anatakiwa kuja na  uthibitisho wa maendeleo ya afya yake.

“Mdhamini wa Lissu utatuletea uthibitisho wa afya ya Lissu ili tuweze kuweka kwenye rekodi zetu,”alisema Simba.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Simba ameahirisha shauri hilo hadi Novemba 21 2019 itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Mbali
na Lissu washtakiwa wengine ni Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina,
Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Inadaiwa
kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir,
Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye
kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’