Masauni apiga marufuku mawakili nje ya ofisi za nida

Na Mwandishi Wetu

Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni amepiga
marufuku watu wanaojiita mawakili na kuwatoza wananchi kiasi cha  fedha
kinachozidi shilingi Elfu Kumi  wakidai ni ada ya kupewa nyaraka mbadala
ya cheti cha kuzaliwa ikiwa ni hitajio la msingi kwa wananchi wanaofika
ofisi mbalimbali nchini za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA)

Akizungumza
baada ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa Mkoa wa Morogoro
walioitaka Serikali kuweka bayana kama kupata vitambulisho vya taifa
lazima ulipe hela,Naibu Waziri Masauni alisema vitambulisho hutolewa
bure hakuna haja ya kulipa gharama yoyote huku akipiga marufuku wananchi
kutozwa fedha nje ya ofisi za NIDA

“Kuanzia
sasa kila Ofisi ya NIDA itakuwa na mawakili wa serikali wataohusika na
kuandaa pamoja kuhakiki nyaraka mbalimbali za wananchi wanaokuja kwa
ajili ya vitambulisho vya taifa na ninatoa maelekezo kwa nchi nzima
katika ofisi za NIDA kuwaondoa watu wanaowaandalia wananchi nyaraka hizo
kwanza hatuwatambui kama ni maafisa sheria sahihi au la na wanaweza
kuwathibitisha watu ambao sio raia wakapata vitambulisho kama raia”
alisema Masauni

Akizungumza
katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amesema wao
kama mkoa wako tayari kuleta mawakili wa serikali katika ofisi hizo za
NIDA huku akiwaasa wananchi kwenda sehemu sahihi wanapofika kutafuta
vitambulisho katika ofisi hizo.

“Serikali
ipo kuhakikisha zoezi la utolewaji namba na vitambulisho vya taifa
linamalizika ndani ya siku 20 zilizoongezwa na Rais Magufuli na kama
mkoa tunayafanyia kazi maelekezo ya Naibu Waziri Masauni na kuanzia
kesho mawakili wa serikali watakuwepo hapa kuhakiki na kutengeneza
nyaraka za serikali kwa wananchi” alisema RC Sanare

Nae
Afisa Usajili wa  NIDA Mkoa wa Morogoro,James Malimo amesema katika
Mkoa wa Morogoro na Wilaya zake jumla ya vitambulisho 347,466 kati ya
849,436 vimezalishwa huku maombi 237.236 yakikwama kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo waombaji kukosa vigezo vya uraia,mihuri ya wadau na
viambata.