Mawakala wanaotumiwa na wazalishaji wa vifaranga vya kuku wakamatwe kama hawajasajiliwa-ndaki

 

Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Mashimba Ndaki akizungumza na wauzaji wa kuku
wa nyama na wazalishaji wa vifaranga baada ya kuwakutanisha na kueleza
changamoto zao.Kikao hicho kimefanyika leo katika ofisi za wizara hiyo
Jijini Dar es Salaam.


Msajili
wa Bodi ya Nyama Bw.Imani Sichwale akizungumza na wafanyabiashara wa
kuku wa nyama pamoja na wazalishaji wa vifaranga vya kuku. Kikao hicho
kimefanyika leo katika ofisi za wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM




Chama
cha wafugaji wa kuku wa nyama TABROFA kimetakiwa kuwa na ushirikiano wa
kutosha ili kuweza kutokomeza changamoto wanazozipata wafanyabiashara
wa kuku hasa Mawakala wasiotambulika wanaouza vifaranga vya kuku wa
nyama pamoja na vyakula vya kuku katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es
Salaam.


Akizungumza
katika mkutano wa Wafanyabiashara na wazalishaji wa vifaranga vya kuku
wa nyama Jijini Dar es Salaam Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Mashimba
Ndaki amesema mawakala wanaotumiwa na wenye viwanda vya kutotolesha
vifaranga kama hawajasajiliwa wakamatwe.


“Kuanzia
sasa mawakala wa wauzaji wa vifaranga vya kuku pamoja na chakula cha
kuku nataka wafuatiliwe na waeleze wapi walisajiliwa”. Amesema
Mhe.Ndaki.


Aidha,
Mhe.Mashimba amewataka wafugaji wote wanaouza kuku wa nyama kujisajili
Bodi ya Nyama kwa ajili ya biashara kwani hatua kali za kisheria
zitachukuliwa kwa atakayekaidi.


Pamoja
na hayo Mhe.Ndaki amesema sekta ya ufugaji ni muhimu kwa pato ya nchi
na kuwataka wataalamu wa mifugo kufanya tafiti za mifugo kwa kuwalenga
wafugaji wenyewe kwa kubaini changamoto zao sio kuwatumia wasomi.


“Tuache
kufanya tafiti kwa kuwatumia bwanashamba na bibishamba ambao
hawafikishi ujumbe kwa wafugaji kuhusu elimu dhidi ya tafiti
zilizofanyika,” ameeleza.


Naye
Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Bw.Imani Sichwale aliwataka wafugaji hao
kuacha kufuga kuku kwa mazoea bali wafuge kitaalamu kwa kuweka bajeti
ya ufugaji kwa lengo la kukuza tasnia yao.


Hata hivyo Sichwale amesema kuwa nyama inasoko nje ya nchi kuliko kuku kwa sababu haijapata vigezo vya uuzaji wa nje ya nchi.


Vilevile
Bw.Sichwale amesema asilimia 80 ya wafugaji wa kuku wa nyama ni
wanawake hivyo amewataka kushikilia tasnia hiyo kwa lengo la kuondoa
umaskini kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa ujumla.


Kwa
upande wake Mwenyekiti wa chama cha wafugaji wa kuku wa nyama TABROFA
Bw.Costa Mrema amesema katika tafiti walizozifanya zimebaini kuwa ulaji
wa kuku wa nyama Tanzania ni kati ya kuku laki 9 hadi milioni 1.2 kwa
wiki.


“Idadi
hiyo 70% ya walaji wa kuku wa nyama ni Dar es Salaam na Pwani
ikifuatiwa na mikoa ya Arusha, Mwanza,Kilimanjaro na Dodoma”. Amesema
Bw.Mrema.