Mkoa wa shinyanga wazindua kampeni ya ongea nao kamanda magomi atoa takwimu za ukatili wa kijinsia.

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna
msaidizi wa Polisi Janeth Magomi amesema mpaka sasa kesi za ukatili wa kijinsia
zilizoripotiwa Mwaka huu 2023 ni kesi 105 ambapo Mwaka jana jumla ya kesi 97
ziliripotiwa Mkoani Shinyanga.

Ametoa takwimu hizo kwenye  uzinduzi wa kampeni ya Ongea nao Mkoa wa Shinyanga iliyokwenda sanjari na siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo hafla hiyo  imefanyika 
katika viwanja vya shule ya msingi Buduhe Halmashauri ya Wilaya ya
Kishapu.

Kamanda Magomi amesema kuongezeka kwa kesi za ukatili
wa kijinsia Mkoani Shinyanga ni kutokana na elimu inayoendelea kutolewa kwa
wananchi katika kuripoti kesi za ukatili huku akiwasisitiza wananchi kutofumbia
macho kesi za ukatili wa kijinsia zinazoendelea kufanyika kwenye familia ama
jamii wanayoishi.

Hata hivyo Kamanda Magomi ametumia nafasi hiyo
kuwataka wanafunzi, wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana katika
mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto.

‘Tunawataka
wanafunzi, wananchi na wadau kutambua kuwa mnawajibika na kupaza sauti na kutoa
taarifa za uhalifu katika vyombo vya sheria ili kutokomeza vitendo hivyo katika
jamii inayotuzunguka kwani jukumu la ulinzi na usalama nila kila mwananchi hata
hivyo ni vyema mkatambua kuwa ukatili wa kijinsia ni changamoto kubwa katika
jamii na wahanga wakubwa ni watoto na wanawake hivyo hamna budi kutoa taarifa za
ukatili wa kijinsia kwa wakati ili wahalifu waweze kukamatwa na kuwajibishwa
kwa mujibu wa sheria’
.amesema kamanda Magomi

Kamanda magomi ametaja matendo ya ukatili wa kijinsia
kuwa ni pamoja na ubakaji, ulawiti, kipigo, kutelekeza familia, kutumikisha watoto
na kuwazorotesha masomo, lugha za matusi na ndoa za utotoni.

Amesema madhara ya ukatili wa kijinsia ni pamoja na
vifo, mimba za utotoni, maradhi yanayosababishwa na ngono mfano UKIMWI, ulemevu
wa kudumu, kuongezeka kwa watoto mtaani, umaskini, msongo wa mawazo na
mmomonyoko wa kifamilia.

Pia amewataka wananchi kutambua mifumo mbalimbali ya
utoaji wa taarifa za ukatili wa kijinsia mifumo hiyo ni pamoja na dawati la
jinsia na watoto Polisi, viongozi wa Dini, ustawi wa jamii, viongozi wa
serikali za mitaa au mtu yoyote anayeaminika kwenye jamii hiyo.

Kamanda Magomi ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa
Shinyanga kuungana kwa pamoja katika kampeni ya Ongea nao hususan kwenye
masuala ya kutoa elimu kwa wananchi wa lika zote ili Mkoa wa Shinyanga uendelee
kuwa salama.

Akizungumza mgeni rasmi katika hafla hiyo, katibu
tawala wa Wilaya ya kishapu Bi. Fatma Mohamed pamoja na mambo mengine
amewakumbusha wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na serikali
katika kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa kutoa taarifa ili kufikia malengo ya
usawa wa kijinsia.

Baadhi ya wadau mbalimbali wa kupambana na ukatili
akiwemo mwakilishi kutoka kampeni ya SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga pamoja na
mwakilishi kutoka kampeni ya sauti ya watoto Tanzania wamesema wataendelea
kuibua na kutokomeza ukatili unaoendelea katika familia na jamii kwa ujumla.

Mtandao wa Polisi wanawake Tanzania (TPF – NET) Mkoa wa Shinyanga leo Disemba 1,2023 umezindua  kampeni ya Ongea nao ambayo inatekelezwa na
Polisi wanawake Mkoa wa Shinyanga ambapo mwenyekiti wa mtandao huo Mkoa wa Shinyanga ni RPC Janeth Magomi. 

Kauli mbiu yake inasema “Wekeza
kuzuia ukatili wa kijinsia” na ‘Polisi jamii kwa usalama na maendeleo yetu”
ambapo lengo lake ni kutoa elimu kwa vijana, wazee, watoto kuhusu masuala ya
usalama wa raia na mali zao, ukatili wa kijinsia, mauaji pamoja na mmomonyoko
wa maadili. 

Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania
(TPF-NET) Mkoa wa Shinyanga baada ya kuzindua kampeni ya “ONGEA NAO” umegawa  taulo za kike na madaftari kwa wanafunzi, kutoa
mahitaji mbalimbali kwa watu wenye uhitaji kaya 50 katika kata tatu za Wilaya
ya Kishapu,kutoa msaada wa kilo 250 za mchele, Sabuni miche 50, Sukari kilo
100, Maharage kilo 100 na mafuta ya kupikia kilo 50.  

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna
msaidizi wa Polisi Janeth Magomi ambaye pia ni mwenyekiti wa TPF – NET Mkoa wa
Shinyanga akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Ongea nao Mkoa wa
Shinyanga iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Buduhe Halmashauri ya
Wilaya ya Kishapu.

Mgeni rasmi, katibu tawala wa Wilaya ya kishapu Bi.
Fatma Mohamed akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampeni ya Ongea nao Mkoa
wa Shinyanga iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Buduhe Halmashauri
ya Wilaya ya Kishapu.



Mgeni rasmi, katibu tawala wa Wilaya ya Kishapu
Bi. Fatma Mohamed akiendelea na zoezi la kugawa msaada wa vitu mbalimbali
ikiwemo  taulo za kike na madaftari kwa
wanafunzi, mahitaji mbalimbali kwa watu wenye uhitaji kaya 50 katika kata tatu
za Wilaya ya Kishapu.