Mwekezaji kutoka india aonesha nia kuwekeza kilimo cha mpunga, kiwanda cha kuchakata mpunga simiyu

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Mwekezaji
kutoka nchini India, Bw.Vivek Agarwala ameonesha nia ya kuwekeza kwenye
kilimo cha mpunga kupitia umwagiliaji na kujenga kiwanda cha kuchakata
mpunga wilayani Busega mkoani Simiyu, ambapo anatarajia kuwekeza katika
eneo lenye ukubwa wa ekari zipatazo 2000.

Akizungumza
na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Simiyu baada ya kutembelea maeneo
mbalimbali yenye fursa ya uwekezaji katika kilimo cha mpunga wilayani
Busega, Bw. Agarwala amesema mkoa wa Simiyu na Tanzania kwa ujumla ina
rasilimali nyingi hivyo ikiwa Makampuni kutoka India yatafanya kazi kwa
kushirikiana na Watanzania rasilimali hizo ziatakuwa na manufaa kwa
Watanzania.

“Mkoa
wa Simiyu na Tanzania kwa ujumla ina rasilimali za kutosha ambazo zipo
kwa ajili ya kuwanufaisha Watanzania wenyewe hivyo  kinachohitajika ni
teknolojia, uwekezaji, ushirikiano kutoka Serikalini kufanya haya yote
yatokee; baada ya ziara hii ninaamini tukiyatekeleza kwa juhudi yale
tuliyokubaliana mkoa huu utaendelea kwa kasi,” alisema Agarwala.

Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amemhakikishia mwekezaji huyo
upatikanaji wa eneo la ekari 2000 kwa ajili ya uwekezaji na kubainisha
kuwa malengo ya mkoa ni kuhakikisha wilaya ya Busega inakuwa mzalishaji
mkuu wa chakula katika mkoa kwa kuwa ndiyo wilaya yenye ziwa Victoria
ndani ya Mkoa.

Aidha,
pamoja na kutoa ushirikiano kwa mwekezaji kutimiza azma yake Mtaka
amesema Serikali ya Mkoa imezungumza na Benki ya CRDB kuona uwezekano wa
kuwawezesha wakulima wa mpunga wilayani Busega hususani walio kando ya
ziwa Victoria kupitia dirisha la kilimo ili waweze kulima kisasa kupitia
umwagiliaji.

Naye
Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa, Bw. Lusingi Sitta amesema Benki
iko tayari kumuunga mkono mwekezaji na wakulima wa wilaya ya Busega 
kupitia dirisha la kilimo kutokana na wilaya hiyo kuwa na maeneo mazuri
na chanzo cha uhakika cha maji (Ziwa Victoria), ambapo alibainisha kuwa
tayari benki hiyo ina uzoefu wa kuwezesha miradi mbalimbali ya kilimo
cha umwagiliaji.

Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu,
Mhe. Enock Yakobo amesema wao kama chama wanaunga mkono juhudi za watu
wanaoitika huku akiongeza kuwa mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayofanya
vizuri kwenye kilimo hususani cha mpunga hivyo ujio wa mwekezaji huyo
mkoani hapa utasaidia kuongeza tija kwenye zao hilo.

Katika
hatua nyingine  baadhi ya wakulima wamesema kuwa ujio wa mwekezaji 
huyo utawasaidia wao kuzalisha kwa tija ikilinganishwa na awali,”
tukianza kulima kilimo cha umwagiliaji tunaamini tutavuna mavuno mengi
maana tutalima zaidi ya mara moja kwa msimu” alisema Monika Msabila

“Kuna
kipindi mavuno yanashuka kama mvua zikiwa chache sasa ujio wa mwekezaji
huyu tumeupokea maana atatusaidia na sisi kulima kilimo cha umwagiliaji
na kuacha kutegemea mvua pekee ” alisema Simon Ngelela mkazi wa Kijiji
cha Shigala wilayani Busega.

Katika
hatua nyingine mwekezajI alipata fursa ya kutembelea kiwanda
kinachomilikiwa na Mwekezaji mzawa, Deogratius Kumalija ambacho
kinaongeza thamani kwenye mazao ya chakula hususani mpunga na mahindi
Busega Mazao Limited  kilichopo wilayani Busega.