Naibu waziri mabula aimwagia sifa nhc katavi

Na Munir Shemweta, WANMM KATAVI

Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Katavi kwa kuwa
moja ya mkoa wenye miradi mingi ya Shirika hilo.

Dkt
Mabula alitoa pongezi hizo jana wakati akikagua miradi ya NHC kwenye
mkoa wa Katavi akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta
ya ardhi pamoja na ujenzi wa miradi inayotekelezwa na  Shirika la
Nyumba la Taifa.

Miradi
aliyoikagua Naibu Waziri Mabula katika mkoa wa Katavi ni ujenzi wa
nyumba za watumishi katika Halmashauri ya wilaya ya Mlele, Ofisi na
Nyumba ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na ukumbi wa
halmashauri ya Manispaa ya Mpanda. Pia alikagua mradi wa nyumba sabini
za Ilembo ambapo Nyumba kumi kati ya hizo ziliuzwa na nyumba sitini
zimepangishwa.

Alisema,
mkoa wa Katavi unaweza kuwa mkoa wa kwanza ama wa pili kwa kuwa na
miradi mingi ya Shirika la Nyumba la Taifa na hali hiyo siyo tu
inaonesha jinsi Shirika lilivyo makini kwenye uwekezaji miradi
mbalimbali kama vile ujenzi wa nyumba za kuuza, kupangisha na majengo ya
biashara bali inalifanya kuimarika kimkoa.

Akigeukia
mradi wa Jengo la Biashara la Paradise lililopo Manispaa ya Mpanda, Dkt
Mabula alilisifu jengo hilo kwa kuwa na mazingira mazuri ya kibiashara
na kushauri taasisi za serikali katika mkoa wa Katavi kutumia fursa ya
kupanga na kuwekeza kwenye jengo hilo kwa kuwa gharama zake ni nafuu
ukilinganisha wapangishaji wengine.

Aidha,
amelitaka Shirika la NHC mkoa wa Katavi kuhakikisha inalifanyia
matangazo jengo hilo la biashara la Paradise kwa lengo la kuvutia wateja
kupanga hasa ikizingatiwa kutolitangaza kunaweza kusababisha kukosa
wateja.

Kauli
hiyo ya kutaka kufanyika matangazo kwenye jengo hilo inafuatia Naibu
Waziri Mabula kuelezwa na Kaimu Meneja wa Shirika la NHC  mkoa wa Katavi
na Rukwa Masumbuko Majaliwa kuwa mpaka sasa jengo hilo la kibiashara
limepangisha asilimia thelathini tu ya wateja.

‘’Mrudi
kwenye kutangaza miradi yenu kupitia kipindi cha Maisha ni Nyumba na
ikiwezekana kazi hiyo ifanyike mkoa kwa mkoa na mhakikishe miradi yenu
mnaifanya kwa kasi, viwango na wakati ili kujenga trust kwa wateja’’
Alisema Dkt Mabula.

Kwa
upande wake Meneja Mawasiliano wa NHC Muungano Saguya alisema, kwa sasa
Shirika lake linafanya vizuri katika masuala ya ujenzi jambo
lililosababisha kuaminwa na serikali ambapo katika mji wa serikali eneo
la Mtumba Dodoma liliweza kujenga majengo ya Wizara nne na sasa Shirika
linaendelea na utekelezaji wa miradi mingine kama vile ujenzi wa nyumba
na ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) nchi nzima.

Awali
Kaimu Meneja wa Shirika la Nyumba mkoa wa Katavi na Rukwa Masumbuko
Majaliwa alimueleza Naibu Waziri kuwa kwa sasa NHC mkoa wa Katavi
inatekeleza miradi mbalimbali katika mikoa ya Katavi na Rukwa.

Alisema
katika mkoa wa Katavi Shirika la Nyumba linatekeleza miradi ya nyumba
za watumishi Mlele, ukumbi wa manispaa ya Mpanda pamoja na ujenzi wa
nyumba za walimu Kibaoni wakati upande wa mkoa wa Rukwa miradi
inayotekelezwa ni ile ya mradi wa nyumba za makazi jangwani Sumbawanga
pamoja na duka la dawa katika hopspitali ya rufaa mkoa wa Rukwa.