Picha : ajali ya basi na hiace kugongana uso kwa uso yaua na kujeruhi kahama

Na Adela Madyane – Malunde 1 blog Kahama
Watu wawili wamefariki dunia na wengine
saba kujeruhiwa vibaya kutokana na ajali  iliyohusisha basi la Napol
Express kugongana uso kwa uso na Hiache katika eneo la Karagwa Kata ya
Ntobo Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.



Ajali hiyo imetokea baada ya gari aina
ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T 440 DHJ iliyokuwa ikielekea
Kijiji cha Kakola Kata ya Bulyanhulu Halmashauri ya Msalala ambapo
wakati Hiace ikikata kona majira ya usiku ilikutana na basi la Napol
Express yenye namba za usajili T 155 CKG hali iliyopelekea kugongana
uso kwa uso na kusababisha watu wawili kufariki dunia hapo hapo na
wengine saba kujeruhiwa vibaya.

Aidha kwa mujibu wa vyanzo vyetu
vinaeleza kuwa gari hiyo aina ya Toyota hiace kutokana na kutembea huku
ikiwasha taa moja ndiyo chanzo cha kugongwa na basi ubavuni upande wa
kulia na kwamba wakati ajali hiyo ikitokea basi lilikuwa ikitokea
Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza kuelekea Wilayani Kahama.

Jummane Kisendi ni mwenyekiti wa
kitongoji cha Kalagwa, Kata ya Ntobo Halmashauri ya Msalala Wilayani
Kahama akizungumza na Malunde 1 blog alisema kuwa yeye ni shuhuda wa
tukio hilo na hivyo baada ya tukio hilo alitoa taarifa na kuwapigia
simu polisi na hospitali ya Halmashauri ya mji wa Kahama ili kutoa
msaada zaidi na kuokoa maisha ya abilia hao.

Kaimu mganga mfawidhi wa Hospitali ya
Halmashauri ya Mji wa Kahama Dk. Antar Fereji akizungumza  na
waandishi wa Habari alisema kuwa Januari 20 mwaka huu majira ya saa
mbili usiku walipokea miili ya watu wawili waliofariki dunia katika eneo
la ajali na wengine 7 kujeruhiwa vibaya kutokana na ajali hiyo.

Dk. Antar Fereji aliwataja watu
waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Dephina Muluno (30) na Fundi
Saidi (34) wote wakiwa wanawake, na kuongeza kuwa miili hiyo imekwisha
tambuliwa na ndugu na imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti
kwaajili ya taratibu zingine za mazishi.

Akizungumzia upande wa majeruhi alisema
kuwa kati ya watu saba wanawake ni wanne waliojulikana kwa majina ya
Lucia Ndala (7), Kulwa Hamisi (20), Zainabu Ramadhani (42), na Kalekwa
Hangaiki(33) wote kutoka Kakola, huku wanaume wakiwa watatu Abdul Saidi
(15) kutokea Arusha, Ramadhani Abas (20) kutokea Niyogo na Juma Enos
(38) kutokea Busoka Halmashauri ya mji wa Kahama.

Dk Fereji alisema kuwa kutokana na
wagonjwa kuwa na majeraha makubwa watahamishiwa katika Hospitali ya
Rufaa Bugando Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi ambapo watu watano ni
pamoja na Kulwa Hamisi, Zainabu Ramadhan,Kalekwa Hangaiki, Ramadhan
Hamisi na Juma Enos watasafirishwa.

Akizungumzua ajali hiyo, dereva wa
Toyota hiace Juma Enos, ambaye pia ni miongoni mwa majeruhi alisema
kuwa alipata ajali hiyo alipokuwa akipanda mlima katika eneo la
kitongoji cha Kalagwa, alipokutana na basi ambalo lilikuwa mwendo kasi
na kukiri ajali hiyo ilisababishwa na gari zote mbili kuwasha taa moja
ambapo wote walihisiana kuwa ni boda boda na hivyo hiace kukwanguliwa
upande wa ubavuni kulia na kusababisha ajali hiyo.

Akielezea mkasa huo zaidi dereva huyo
alisema kuwa gari lake lilikuwa na taa moja ya upande wa kushoto na
hivyo kumchanganya dereva wa basi aliyeamini mbele yake kuna pikipiki na
sio gari.

Naye
Abdala Saidi (15) mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya
Sekondari mwalimu Nyerere iliyoko Kata ya Segese ameeleza kwamba huenda
ajali hiyo ikakatiza ndoto za masomo yake kwani alikuwa akitokea Jijini
Arusha akielekea Segese kuanza Masomo yake ya kidato cha kwanza.


Muonekano wa Hiace baada ya ajali


Basu la Napol Express

Muonekano wa hiace upande wa pili