Raia wapya wa nsimbo wameanza ujenzi wa sekondari

Mbunge wa jimbo la Nsimbo Richard Mbogo (mwenye nguo ya
mistari) akikabidhi saruji kwa wakazi wa kata ya Ivungwe kwa ajili ya
ujenzi wa shule ya sekondari

Zoezi la uchimbaji wa msingi wa shule ya sekondari Ivungwe katika halmashauri ya Nsimbo likiendelea
……………………

Raia wapya wa tanzania wanaoishi katika kata ya ivungwe katika makazi ya wakimbizi ya katumba katika halmashauri ya nsimbo mkoani katavi wameamua kuanza ujenzi wa shule ya sekondari kwa nguvu zao wenyewe ili kuwaepusha watoto wao kutembea umbali mrefu na kuishi katika nyumba za kupanga hali ambayo inachangia wanafunzi wengi wa kike kushindwa kumaliza shule kwa kupata mimba

Wakizungumzia ujenzi huo wakazi wa kata hiyo wamesema shule hiyo itaweza kuhudumia wanafunzi wa vijiji vitano

Bi. Prota Antony ni mkazi wa kijiji cha ivungwe akizungumzia adha wanazopata wanafunzi wanaosoma katika shule ya sekondari kenswa amesema watoto wa kike wanashindwa kuwahi shule kwa kuogopa kutoka mapema nyumbani kwa kuhofia kubakwa

Ameongeza kuwa kutokana na wazazi wengi kutokuwa na uwezo wa kuwanunulia watoto baiskeli wanafika shule wakiwa wamechoka na hivyo kulala madarasani

Aidha kwa wale waliopangisha vyumba katika mageto wanajikuta wanalazimika kujiuza kutokana na kutokuwa chini ya uangalizi wa kutosha na kupelekea mimba za utotoni

Amesema shule hiyo ikikamilika itasaidia watoto wao kusoma karibu hivyo kuongeza idadi ya wahitimu wa elimu ya sekondari na kuwaepusha na madhara mbalimbali yanayotokea kutokana na kusoma mbali na nyumbani

Katika kuwaunga mkono wananchi hao; vijana wa Katumba wanaoishi katika mikoa mbalimbali hapa nchini; wametoa saruji tani saba na nusu iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 3 laki tano na elfu hamsini kuchangia ujenzi huo

Bwana Wilson Elia ni Mwakilishi wa vijana wa Katumba wanaoishi katika mikoa mbalimbali, amesema wamefikia hatua hiyo katika kuchangia elimu ili wadogo zao wasome katika mazingira mazuri

Wameongeza kuwa wako tayari kuendelea kuchangia katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika kata yao na hata nje ya kata hiyo

Nae diwani wa kata ya Katumba Seneta Baraka amesema shule hiyo itasaidia kupunguza msongamano kwani kata nzima ya katumba yenye wakazi zaidi ya 33,000 ina shule mbili tu za sekondari

Aidha ameahidi kuwa mstari wa mbele katika kusimamia ujenzi wa shule hiyo mpaka kukamilika kwake

“Tunategemea mwezi wa kwanza mwaka 2020 tutaingiza watoto wa kidato cha kwanza hapa” alisema

Ameongeza kuwa awali walikubaliana na wananchi kufyatua tofali za kuchoma lakini walibadilisha maamuzi hayo na sasa watajenga kwa matofali ya saruji

Akikabidhi msaada huo mbunge wa jimbo la nsimbo bwana richard mbogo amewataka wananchi kusimamia huo ujenzi kwa uangalifu mkubwa

Mbogo amewashukuru wananchi kwa kuona umuhimu wa kuwa na shule ya sekondari katika maeneo hayo kwani itapunguza changamoto mbalimbali wanazopata wakipata

Amewataka kuwa jicho la kila mmoja wao na kuhakikisha hakuna mali ya ujenzi inayopotea ili kufanikisha lengo lao

Pia ameshiriki katika uchimbaji wa msingi wa vyumba vya madarasa katika eneo hilo inapojengwa shule hiyo