Rais magufuli atoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya ulinzi wa taifa

Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ametoa shilingi Bilioni 10 kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa
katika eneo la Kikombo Jijini Dodoma.


Mhe.
Rais Magufuli ametoa fedha hizo  tarehe 25 Novemba, 2019 baada ya
kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo na ameagiza milima yote
inayozunguka eneo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa lenye ukubwa wa
ekari 5,567 imilikiwe na JWTZ kwa ajili ya shughuli za ulinzi.

Kuhusu
madai ya fidia, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la
Dodoma Bw. Godwin Kunambi kuwalipa fidia ya shilingi Bilioni 3 na
Milioni 339 wananchi 1,500 wa Kata ya Kikombo ambao ardhi yao
imechukuliwa na JWTZ kwa ajili ya Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa,
kuanzia tarehe 01 Desemba, 2019.

Pamoja
na agizo hilo, Mhe. Rais Magufuli amewatahadharisha wananchi wa Kikombo
kujiepusha na matapeli wanaowahamasisha kudai fidia wasiyostahili kwa
mujibu wa sheria ama kudai ardhi isiyo yao.

Mhe.
Rais Magufuli pia ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
kujenga kwa kiwango cha lami kilometa 18 za barabara inayounganisha
Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa na barabara kuu ya Dodoma – Morogoro.

Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen.
Venance Salvatory Mabeyo aliyeomba Serikali ibebeba jukumu la kulipa
deni la takribani shilingi Trilioni 1 ambalo JWTZ inadaiwa baada ya
kujengewa nyumba 6,064 za makazi ya Askari katika maeneo mbalimbali
nchini, badala ya Askari kukatwa posho zao ili kupata fedha za kulipia
deni hilo kama ilivyowekwa katika mkataba wa ujenzi.

“Nakuhakikishia
hakuna kukatwa Askari yeyote, hilo deni litabebwa na Serikali, kabla
sijaja hapa nimeshamwelekeza Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu, na nafikiri
kesho au keshokutwa wataanza kulipia hilo deni ambalo limeanza kuiva,
tutaanza kulipa Dola za Marekani zaidi ya Milioni 25 (sawa na shilingi
Bilioni 56 na Milioni 948). Mkataba ni kweli ulikosewa, nafikiri ilikuwa
ni mwaka 2012/13 lakini siwezi kukubali makosa ya namna hiyo
yakafanyika katika kipindi changu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Maafisa na Askari wa JWTZ kwa kazi
nzuri ya kulinda mipaka ya nchi na kushiriki katika operesheni za
kulinda amani katika Mataifa mbalimbali, majukumu ambayo yamelijengea
heshima jeshi hilo na Tanzania.
Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo wamemshukuru
Mhe. Rais Magufuli kwa maelekezo yake ya kujengwa Makao Makuu ya Ulinzi
wa Taifa katika eneo la Kikombo ambayo yanajengwa na jeshi lenyewe.

Mapema
kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Mhe. Rais Magufuli ameweka
jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja wa maadhimisho ya kitaifa katika
eneo la Chamwino.
Ujenzi
wa uwanja huo utakamilika Januari 2020 ukiwa na uwezo wa kuchukua watu
5,000 kwa gharama ya shilingi Bilioni 2, na awamu ya pili itahusisha
ujenzi wa ukumbi wa mikutano, jengo la watu mashuhuri na jengo la
kupumzikia watu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino