Rc mnyeti aagiza walioporwa ardhi kiteto wapewe maeneo mbadala


MKUU wa Mkoa wa
Manyara, Alexander Pastory Mnyeti ameagiza wakazi wawili wa Wilaya ya
Kiteto walionyang’anywa maeneo yao na kujengwa  taasisi za Serikali
wapewe maeneo mengine. 
 

Mnyeti alitoa agizo
hilo kwenye mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wananchi wa kata za
Matui na Bwawani, wilayani Kiteto kwenye ziara yake ya siku tano ya
kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza kero na changamoto za wananchi,
kuyapatia majawabu na kuzungumza na wananchi. 
 

Alisema kutokana na
maeneo ya wananchi hao kuchukuliwa na taasisi za serikali na kujengwa
shule ingetakiwa wapewe maeneo mengine ili kufidia maeneo yao. 
 

“Mkurugenzi nakuagiza
utoe maeneo mengine wapewe hawa wananchi waliochukuliwa maeneo yao kwa
ajili ya kufidiwa kwani japo ni suala la maendeleo lakini wanapaswa
kupata haki zao. 
 

Alisema baadhi ya
kero ambazo hazina sababu ya kuachwa zinapaswa kutatuliwa kwani wananchi
wengine wataichukia serikali yao bila sababu ya msingi. 

Awali, mkazi wa
kijiji cha Matui Juma Masare alilalamikiwa kuporwa eneo lake ekari 12 na
serikali ya kijiji kisha ikajengwa shule ya msingi. 
 

“Baada ya kupora eneo
langu serikali ya kijiji ilijengwa shule lakini hawakunifidia sehemu
nyingine japokuwa maeneo mengine yapo,” alisema Masare. 
 

Kwa upande wake,
mkazi wa kijiji cha Wezamtima kata ya Bwawani, Endeni Kilangi alitoa
malalamiko kwa mkuu huyo wa mkoa kuwa alinyang’anywa na serikali ya
kijiji hicho ekari zake 70 na kujengwa shule ya msingi. 
 

“Shamba hilo
lilichukuliwa na serikali ya kijiji lakini sikufidiwa eneo lingine
sehemu nyingine ili hali kuna maeneo mengine wangeweza kunipa haki
yangu,” alisema Kiangi. 
 

Baada ya uamuzi huo wananchi hao walimpongeza Mnyeti kwa kusimamia haki zao kwani ilikuwa ni haki yao kupatiwa maeneo mengine.