Ujerumani yamwanga mabilioni nhif

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James akisaini Mkataba wa Msaada wa Shilingi Bilioni 20 Kati yake na  Kaimu Balozi wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani Bw.Jorg Herrera, Shughuli iliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Doto James na Kaimu Balozi Bw. Jorg Herrera Wakionesha nakala
za Mikataba ya Msaada baada ya kutia saini  Shughuli iliyofanyika katika
Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. (picha zote na Idara ya
Habari –MAELEZO)
………………………….
Na.Mwandishi Wetu –MAELEZO.

Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani
limetoa msaada wa Euro milioni 8 ambazo ni sawa na  shilingi Bilioni 20
kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwaajili ya kuboresha
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)  katika mfuko wa Bima ya
Afya nchini NHIF.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam
katika hafla ya utiaji saini wa msaada huo, Kaimu Balozi wa Ujerumani
nchini Bw.Jorg Herrera amesema msaada huo ni kwaajili ya kuimarisha
mfuko wa Bima ya Afya ili uweze kuwahudumia watanzania wengi zaidi hasa
wale wa vijijini.

Amesema lengo la Shirikisho la
Jamhuri  ya Ujerumani ni kuisaidia Serikali ya Tanzania katika azma yake
ya kuboresha utoaji wa huduma  kwa wanachama wa mfuko wa Bima ya Afya
ili hatimaye kufikia lengo la kutoa huduma ya Afya kwa wote . 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara
ya Fedha na Mipango Bw.Doto James amesema msaada huo umekuja wakati
muafaka ambapo Serikali ya Awamu ya Tano inajitahidi kuboresha huduma za
Afya kwa wananchi wake ili waweze kufanya kazi kwaajili ya kuelekea
Tanzania ya Viwanda.

“Msaada huu ni wa masharti nafuu
kabisa na hatulazimiki kulipa fedha yoyote, na sisi kama Serikali
tumeupitia na kujiridhisha kwamba hauna chembe yoyote ya masharti ndio
maana leo hii tumetoka hadharani kusaini ” Alisema.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya
Fedha alisema msaada wowote ambao serikali inapatiwa hupitiwa na
wataalam makini ambao wanahakikisha hakuna masharti ambayo yatakuja
kusumbua baadaye na pia ni kwa kuzingatia Sheria na Katiba ya nchi.Pia
amesema kwa upande wa Ujerumani wamekuwa marafiki wazuri sana ambao mara
kwa mara wameendelea kuisidia Serikali katika masuala mbalimbali ya
maendeleo.

Aidha Bw. James amesema
uimarishaji wa mfumo wa TEHAMA katika mfuko wa Bima ya Afya una manufaa
makubwa ikiwemo,kuongeza usajili wa wanachama wa bima ya Afya
ikiwajumuisha walioko kwenye sekta isiyo rasmi pia kuboresha namna ya
kuwatambua ,kuwasajili na kuwalipa watoa huduma.

Faida nyingine ni kuboresha
utendaji wa Mfuko wa Bima ya Afya kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA katika
shughuli zake za kila siku pamoja na kuwajengea uwezo wa watumishi wa
mfuko wa  Bima ya Afya.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imeazimia kutoa huduma za Afya kwa wote na ili kufikia lengo
hili, kuna mpango wa kuwa na mfuko mmoja wa Bima ya Afya utakaojulikana
kama “Single Health Insurance Fund” (SNHIF) ambapo itakuwa ni lazima
kila mtanzania kujiunga.

Serikali ya ujerumani siyo mara ya
kwanza kuisaidia Tanzania, kwani imekuwa ikisaidia katika sekta za
Maji, Nishati,Uhifadhi wa maliasili,Usimamizi wa fedha za umma pamoja na
kuijengea uwezo Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. 

Hivi karibuni Serikali ya Tanzania
imeshuhudia mashirika ya kimataifa nchi mbalimbali pamoja na wahisani
wakiendelea kumimina misaada kwaajili ya shughuli za maendeleo kutokana
na uongozi wa Rais Dkt.John Magufuli , ambao umejitahidi kupambana na
ufisadi na kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya wengi.