Rc singida ashauri jeshi la polisi kuanzisha dawati la upimaji macho

Mtaalamu wa macho kutoka  Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Sight Saver akimwelekeza jambo Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi wakati akimpima macho katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani uliofanyika mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick.





Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi ,
akipuliza kifaa cha utambuzi wa kilevi kwa dereva aliyekunywa pombe.
Kulia ni Katibu Tawala wa mkoa huo, Dkt. Angelina Lutambi.



 Wananchi wakisubiri kupima macho kwenye maadhimisho hayo.



 Uandikishaji majina kabla ya kupima macho ukifanyika.



 Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi , akipata maelezo alipotembelea banda la Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Singida kwenye maadhimisho hayo.



 Uandikishaji majina kabla ya kupima macho ukifanyika.



 Mtaalamu wa macho kutoka  Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Sight Saver akimpima macho mwananchi 



 Mwanahabari wa Shirika la Habari Tanzania (TBC) Mkoa wa Singida, Leonard Manga akisoma maandishi kabla ya kupimwa macho.



 Mkuu  wa
Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, akizungumza kwenye ufunguzi wa
maadhimisho hayo. Kushoto ni Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Singida kwenye maadhimisho hayo, Afande Mwakalukwa.

 


Na Waandishi Wetu, Singida.


 


MKUU wa Mkoa wa Singida Dk.
Rehema Nchimbi, ameshauri Jeshi la Polisi nchini kupitia kitengo chake
cha usalama barabarani kuanzisha ‘dawati maalumu’ la upimaji wa afya ya
macho ili kupunguza ajali zitokanazo na uoni hafifu.


 


Dkt. Nchimbi aliyasema hayo
mwishoni mwa wiki mkoani hapa wakati wa zoezi la upimaji macho
linaloendeshwa na Shirika lisilo la kiserkali la Sightsavers,
linalokwenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya Usalama Barabarani.


 


“Kati ya dawati ambalo
mnatakiwa kuwa nalo kwa sasa ni hili la afya ya macho, niwasihi
shirikianeni na wataalamu wa macho nendeni mkafanye kampeni kubwa ya
afya ya macho…himizeni, tuhimizeni ninyi mkisema jamii itawaelewa na
ajali zote zinazotokana na tatizo hili la uoni hafifu zitapungua,”
alisema Nchimbi.


 


Alisema, tunapoadhimisha
wiki ya usalama barabarani tusisahau kuwa afya ya macho ni kati ya
kipengele na mhimili muhimu katika suala zima la usalama barabarani hapa
nchini.


 


Alieleza kuwa, endapo kila
mtumiaji wa barabara atapatiwa huduma stahiki ya afya ya macho basi ni
dhahiri atakuwa mwangalifu, makini na hatimaye kuweza kupiga hesabu
zinazotakiwa awapo barabarani.


 


Akifafanua umuhimu wa uwapo
wa dawati hilo la upimaji macho, alisema iwapo mtumiaji wa barabara
anakabiliwa na tatizo la macho, mathalani wakati fulani badala ya kuona
gari moja anajikuta anaona mawili au kwasababu huna uoni wa mbali una
uoni wa karibu ukafikiri gari lipo karibu kumbe lipo mbali au kinyume
chake, matokeo yake ni mfululizo wa matukio ya ajali kila kukicha.


 


Alisema wakati mwingine mtu
yupo pembeni ya barabara lakini badala ya kusubiri anaamua kukatisha
barabara akiamini chombo cha moto kilicho kulia kwake au kushoto bado
kipo mbali-alisema yote hayo ni matokeo ya matatizo ya afya ya macho
ambayo kwa pamoja jeshi la polisi na jamii ikiamua tatizo hilo
litamalizika.


 


Dkt, Nchimbi aliongeza kuwa
suala la usalama barabarani halimanishi wale wanaoendesha vyombo vya
moto pekee bali ni kwa watumiaji wote wa barabara husika, ikiwemo
watembea kwa miguu, na kuhimiza kila mtu anapaswa kuchukua tahadhari
wakati wote.


 


“Mtumiaji wa barabara
unapokuwa barabarani hakikisha kwanza macho yako yapo sawasawa, pia
unapaswa kuwa wewe mwenyewe ni dereva unayejiendesha, lakini muendeshe
pia na mwenzako aliye kushoto kwako, kulia kwako na nyuma yako…hii iwe
kwa wote ikiwemo waendesha bodaboda, baiskeli, bajaji, wafugaji, na
vyombo vingine vya moto ili tuweze kumaliza kabisa ajali hizi zinazoweza
kuepukika,” alisema.