Sekta ya ngozi, nyama na maziwa zaundiwa kozi fupi vyuoni

Na. Edward Kondela

Serikali
imewataka wadau kwenye sekta ya ngozi, nyama na maziwa wanaoandaa
mitaala kwa ajili ya vyuo kufundisha kozi fupi katika sekta hizo ngazi
ya cheti na diploma kupitisha mitaala bora itakayohakikisha wanafunzi
watakaohitimu mafunzo wanaleta matokeo chanya katika sekta hizo kwa
wananchi na taifa kwa ujumla.


Akizungumza
Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kilichowahusisha wadau katika
sekta za ngozi, nyama na maziwa kutoka serikalini na taasisi binafsi
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof.
Elisante Ole Gabriel amesema ili kupata malighafi bora zinazotokana na
sekta ya ngozi, nyama na maziwa ni lazima wataalam ambao wamesomea sekta
hizo ngazi ya cheti na diploma wawekewe mazingira ya kuhakikisha
wanatumia utaalam watakaoupata kupitia vyuo mbalimbali baada ya
kupitishwa kwa mitaala hiyo ili iwe na tija kwa taifa.

“Mitaala
mnayokwenda kupitia na kuzungumzia lazima ijibu mahitaji ya wadau
katika sekta tatu yaani ngozi, nyama na maziwa isiwe kuwa na cheti baada
ya kuhitimu mafunzo ngazi ya cheti au diploma hawa wataalamu wa ngazi
ya kati ndiyo wanaotegemewa kwenda kufanya kazi za vitendo, hakikisheni
mnapata mitaala ambayo itakuwa na manufaa.” Amesema Prof. Gabriel

Aidha
Prof. Gabriel amewataka wadau hao kubainisha njia bora za kufundishia
mara baada ya kupitishwa kwa mitaala hiyo ili kuhakikisha wanafunzi
watakaodahiliwa wanaelewa vizuri pamoja na kuwa na utaratibu mzuri wa
kuwapata watu ambao wanafundishika na wawe tayari kupokea mafunzo hayo.

Akibainisha
juu ya jamii kuwa na ufugaji wenye tija, katibu mkuu huyo amewaasa
wadau wa mifugo wajenge utamaduni wa kuwatumia wataalam hususan wa ngazi
ya kati ili waweze kufuga kisasa na kunufaika kupitia mifugo yao badala
ya kufuga kwa mazoea na hatimaye kupata hasara.

Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Utafiti, Ugani na Mafunzo kutoka Wizara ya
Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa amesema mjadala wa kuandaa mitaala
kwa ajili ya kufundisha vyuoni kozi fupi katika ngazi ya cheti na
diploma kwenye kwenye sekta ya ngozi, nyama na maziwa umetoka kwa wadau,
hivyo wizara ikashirikisha taasisi mbalimbali likiwemo Baraza la Taifa
la Elimu ya Ufundi (NACTE) ili kukamilisha mitaala hiyo.

Dkt.
Mwilawa amefafanua kuwa mara baada ya kukamilika kwa taratibu za
kuandaa mitaala hiyo vyuo vya serikali kwa kushirikiana na binafsi
vitaanza kutekeleza kwa kutoa mafunzo ya tasnia ya ngozi, nyama na
maziwa katika ngazi ya cheti na diploma.

Akielezea
umuhimu wa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuandaa mitaala
hiyo, Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania Bw. Magembe Makoye
ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuhakikisha sekta ya mifugo
inasimamiwa vyema kupitia mambo ya kisera na kisheria ambayo ndiyo
yamekuwa yakisimamia pamoja na kutunga kanuni mpya zenye lengo la
kuhakikisha sekta ya mifugo inathaminiwa zaidi.

Bw.
Makoye amesema sekta ya mifugo ambayo inaajiri watu wengi kote nchini
kupitia mafunzo yatakayoanza kutolewa vyuoni mara baada ya kupitishwa
kwa mitaala hiyo kutachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza thamani ya sekta
ya ngozi, nyama na maziwa kwa kuwa wafugaji sasa wataongezewa taarifa
na maarifa kupitia kwa wataalamu watakaohitimu mafunzo hayo.

Wizara
ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya ngozi, nyama
na maziwa pamoja na taasisi mbalimbali likiwemo Baraza la Taifa la Elimu
ya Ufundi (NACTE) inapitia mitaala kwa ajili ya kuanzishwa kwa kozi
fupi ngazi ya cheti na diploma katika sekta hizo kwenye vyuo vya
serikali na binafsi ili kuyaongezea thamani zaidi mazao ya ngozi, nyama
na maziwa kwa kuwa na waatalamu wengi zaidi ngazi ya kati walipobobea
katika sekta za ngozi, nyama na maziwa.