Serikali yasema imejipanga kudhibiti sumu kuvu, kiwanda cha a to z kuanza kuzalisha kidhibiti cha sumu hiyo ‘aflasafe’ na kukisambaza kwa wakulima

Na Seif Mangwangi, Arusha
KIWANDA Cha A to Z cha Jijini hapa
kimesema kiko kwenye taratibu za mwisho za kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha
kiuatilifu aina ya Aflasafe kwaajili ya kuzuia maambukizi ya sumukuvu ambayo
inaelezwa kusababisha madhara makubwa kwa afya za binaadam ikiwemo saratani ya
ini.
 

wajumbe wa mkutano wakiwa katika picha ya pamoja na waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wa tano aliyekaa mbele



Mtendaji mkuu wa kiwanda cha A to Z,
Kalpesh Shah amesema tangu walipoingia mkataba na taasisi ya  Kimataifa ya International Institute for
Transforming African Agriculture (IITA), kutengeneza kiuatilifu hicho
(Aflasafe), tayari wameshawekeza mtaji wa dola za Kimarekani milioni 0.35 na
matarajio ni kutumia dola milioni 1.5 katika miaka mitano ijayo.
Akiwasilisha mada kwenye mkutano wa
kwanza wa Afrika wa kudhibiti Sumukuvu (Aflasafe) kwenye vyakula unaoendelea
kwa siku yake ya mwisho leo jijini hapa, Kalpesh Shah amesema sumu kuvu ni
ngumu sana kuitambua kwenye mazao hivyo zinahitajika gharama kubwa sana
kukabiliana nayo.
Amesema A to Z kupitia taasisi yake ya Africa Research Institute wanayoiendesha kwa ushirikiano na Sumitomo, imekuwa ikipambana kufanya tafiti mbalimbali na kuja na teknolojia mbadala ya kupambana na magonjwa tofauti athari kwa binaadam ikiwemo kutengeneza chandarua chenye kiuatilifu cha kuua mbu wanaoenea ugonjwa wa malaria lakini pia mifuko ya kuhifadhi mazao yasiweze kuharibiwa na wadudu waharibifu.
Akifungua mkutano huo wa Kimataifa
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema Serikali imedhamiria kukabiliana na sumukuvu
kwa kuanzisha tafiti katika mazao ambayo yanaelezwa kukumbwa na ugonjwa huo
ikiwemo mahindi na karanga.
 

Washiriki wa mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja

Amesema katika kuonyesha nia ya
kukabiliana na tatizo hilo,  hivi karibuni,
Serikali ya Tanzania ilipata fedha za kutekeleza mradi wa kuzuia kuenea kwa
sumukuvu hapa nchini (TANIPAC).
Waziri Hasunga amesema lengo la
Serikali ni kupunguza kutokea kwa madhara ya sumukuvu katika mfumo wa chakula
kupitia udhibiti husishi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya mahindi na
karanga, hivyo kuboresha uhakika na usalama wa chakula na hatimae kuimarisha
afya na lishe ya jamii yetu na kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi
zinazotuzunguka.
Mkakati huo unazingatia udhibiti wa
sumukuvu katika hatua za uzalishaji, uvunaji, udhibiti wa kibaolojia,
teknolojia baada ya kuvuna na njia za ukaushaji, uhifadhi, kujenga uwezo wa
kitaasisi, uratibu na kutoa elimu ya kuhamasisha wadau muhimu. Ushiriki wa
sekta binafsi ni muhimu katika uhaulishaji wa teknolojia pamoja na kuhakikisha
mradi unakuwa endelevu.
Waziri Hasunga amesema kuwa
Ushirikiano wa kiutafiti, kati ya sekta binafsi na watunga sera, ni muhimu
katika kufanikisha mageuzi ya kilimo.
Amesema tangu kuibuka kwa tatizo la
sumukuvu mwaka 2016, Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kupunguza kusambaa
kwa sumukuvu hapa nchini kwa kutambua changamoto za kukabili sumukuvu, ambapo
kunahitajika kutumia njia mbalimbali kuanzia kwenye hatua za uzalishaji,
uvunaji, uhifadhi, usindikaji na kuhusisha sekta za Umma na Binafsi katika
kupunguza upotevu wa chakula na kuongeza upatikanaji wa chakula salama na lishe
bora.
Amesema, Tanzania imeanzisha
Kamati  Jumuishi ya Uendeshaji inayohusisha sekta na taaluma kutoka
taasisi mbalimbali chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Kilimo ambayo ina mamlaka ya
kusimamia masuala yote yanayohusu sumukuvu.
Kadhalika, amewahakikishia washiriki
hao kuwa kinga ya sumukuvu – Aflasafe TZ01;  imeshasajiliwa kwa matumizi
hapa nchini Tanzania na kampuni iliyopewa jukumu la kuendesha mradi huo ni
kiwanda cha A to Z kilichokuwepo kisongo jijini Arusha. 
 “Aidha, nimefarijika kuwa kazi hii
inafanywa na Kampuni Binafsi ambayo imewekeza katika uzalishaji, na usambazaji
wa bidhaa hii ambayo itaokoa Maisha ya watu hapa nchini, A to Z ni kiwanda
kikubwa na nina uhakika kazi hii wataifanya vizuri sana,” Alisisitiza
“Napenda kuwahakikishia utayari
wa Wizara yangu katika kuyatumia maazimio mtakayokubaliana katika mkutano huu.
Aidha, Serikali ya Tanzania, inatilia maanani na inaunga mkono hatua
zinazochukuliwa katika kuhimiza biashara ya chakula salama, usalama wa chakula
na lishe” Alisema Waziri Hasunga
Tanzania kwa sasa inatekeleza Awamu
ya Pili ya  Programu ya Uendelezaji wa
Sekta ya Kilimo (ASDP II) yenye lengo la kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo kuwa
na kilimo chenye tija na kibiashara, pamoja na kukuza uchumi wa wakulima wadogo
na kuboresha maisha, uhakika wa chakula na lishe bora.
Uhakika wa chakula na lishe ni
muhimili ambao ni muhimu wa ASDP II Katika kufikia malengo hayo, uwekezaji
katika utafiti wa kilimo ni muhimu katika kuleta matokeo kwa wakulima na wadua
wengine katika mnyororo wa thamani.
Waziri Hasunga amesema kuwa kutokana
na takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) za mwaka
2017, Tanzania inaongoza katika uzalishaji wa mahindi na karanga katika ukanda
wa nchi za Afrika Mashariki, kwa kuzalisha tani milioni 6 na tani milioni moja
mtawalia.
Amesema, Pamoja na mafanikio hayo,
Serikali inatambua kuwa, ingawa mazao hayo ni muhimu kwa chakula cha kila siku,
lakini yanakabiliwa na ukubwa wa tatizo la sumukuvu ambalo linahatarisha
usalama wa chakula na kuwa kikwazo cha biashara ya mazao hayo kwa nchi jirani
na Tanzania.
Mkutano huu ambao umewaweka pamoja
watafiti, wafanyabiashara, watunga sera na wadau wa maendeleo, ambao unalenga
kupanga mikakati ya kuongeza kasi ya matumizi ya kinga ya sumukuvu (Aflasafe),
na kukabili sumukuvu barani Afrika, unadhihirisha mabadiliko chanya ya
kimtazamo tunayoyahitaji.