Egidia Vedasto
APC Media, Arusha.
Shirika la Usawa wa Kijinsia (EFG) linalotoa elimu kwa mwanamke wa Sokoni limewanufaisha wanawake wanaofanya biashara sokoni, kujua haki zao, kupinga ukatili wa kijinsia na kutambua pa kwenda pale wanapofanyiwa vitendo vya kikatili.
Akizungumza katika Wiki ya CSO, Mwenyekiti wa Soko la Kiwalani Jijini Dar es salaam ambaye ameongoza kwa miaka nane mfululizo Neema Mayega, ameipongeza (EFG) kwa elimu wanayoendelea kuwapa wananwake wanaofanya biashara sokoni, hatua ambayo imeinua uchumi wao na taifa kwa ujumla.
“Kabla sijapata elimu ya (EFG) nilikuwa mama wa sokoni nisiyefahamu kama naweza kuwa kiongozi au kutetea haki zangu za msingi pale ninapotendewa kinyume, na vitendo vya ukatili vilikuwa vingi, lakini baada ya elimu hii nilifunguka mno na kuweza kuomba nafasi ya uongozi, nimeaminiwa na leo ninaongoza kwa miaka nane kama Mwenyekiti wa Soko la Kiwalani” amesema na kuendelea
“Nawaomba Taasisi ya Usawa wa Kijinsia msiishie hapo mlipofikia, bali endeleeni kujitanua kwenda mikoa mingine ili kumsaidia mwanamke, aweze kuzijua haki zake, kujitetea na kuwa huru katika mazingira yake ya kazi” ameeleza Bi Mayega.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Equality for Growth (EFG) linalofanya kazi zake Jijini Dar es salaam Jane Magigita amesema mwanamke asipokuwa na mazingira rafiki mahali pa kazi serikali inapoteza mapato na maendeleo yanazorota,
“Naiomba Serikali kurudisha sehemu ya mapato kwa wananchi mfano, unakuta miundombinu sokoni ni mibovu hakuna vyoo wala sehemu za kujisitiri kwa mwanamke, soko lichafu limechakaa wakati huo kodi na ushuru zinakusanywa kila siku” amefafanua Magigita.
Pia Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE lililopo Mkoani Shinyanga linalookoa na kulea mtoto wa kike anayeishi mazingira magumu John Miyola ameipongeza EFG kwa kumkomboa mwanamke hasa yule anayeishi mazingira yenye ukatili.
“Kupitia Taasisi hii tumeimarisha namna ya kutoa huduma na elimu kwa jamii hasa namna ya kuwahudumia wanawake wa sokoni, stendi, viwandani na maeneo mengine” ameeleza Miyola.
Mshiriki wa Wiki ya CSO Mwanafunzi wa Kidato cha tano kutoka Geita Highschool Dorica Asida ametaka wanafunzi kushrikishwa kutoa maoni Dira ya Taifa ya Maendeleo na kuwa miongoni mwa wajumbe katika Bodi za Shule ili maoni yao yafanyiwe kazi na wapate haki zao stahiki.
“Siwezi kusema hatushirikishwi moja kwa moja, lakini maoni yetu hayatendewi haki na wakati mwingine yanatupwa nje badala ya kuzingatiwa, hii yote ni kwa sababu hatupo kwenye Bodi na Kamati za Shule, napendekeza tushirikishwe kikamilifu ili Dira ya maendeleo 2050 iwe na maoni yetu yatakayokuwa endelevu na kuleta mabadiliko chanya kwa miaka hiyo” ameeleza Dorica.