Shule ya msingi lubaga mkoani shinyanga imeshika nafasi ya 10 bora miaka minne mfululizo kwa ufaulu, mfanyabiashara gilitu apata tuzo ya heshima

Mwalimu mkuu wa shule ya
msingi Lubaga Stella Lucas  Halimoja akimkabidhi
cheti cha heshima mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited Bwana
Gilitu Makula kwa lengo la kutambua mchango wake katika kuchochea maendeleo ya
shule ya msingi Lubaga.

Na Mapuli Misalaba,
Shinyanga

Shule ya msingi Lubaga
iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imempa cheti cha heshima
mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited Bwana Gilitu Makula kwa
kuchochea maendeleo na ustawi wa shule hiyo hali iliyosababisha kushika nafasi
ya 10 bora ngazi ya Halmashauri kwa Miaka minne mfululizo.

Hayo yamebainishwa na
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lubaga STELLA LUCAS  HALIMOJA wakati  akisoma risala  kwenye hafla fupi ya kumpongeza na kutambua
juhudi na mchango wa Mfanyabiashara huyo wa Mkoa wa Shinyanga Bwana Gilitu
Makula katika mafanikio,maendeleo na ustawi wa shule hiyo.

Mwalimu Stella amesema
kwa Miaka minne mfululizo shule hiyo imekuwa ikiongeza wastani wa ufaulu katika
matokeo ya mtihani wa darasa la saba,juhudi ambazo zimetokana pia na mchango wa
wadau wa maendeleo akiwemo Mfanyabiashara Bwana Gilitu.

“Kwa
Miaka minne mfululizo tumekuwa tukiongeza wastani wa ufaulu katika matokeo ya
kitaifa ya mtihani wa darasa la saba PSLE ambapo Mwaka 2020 tulikuwa na
watahiniwa 52 tulipata ufaulu wa wastani wa alama 182.6538, Mwaka 2021 tulikuwa
na watahiniwa 52 pia tulipata ufaulu wa wastani wa alama 223.9231, Mwaka 2022
tulikuwa na watahiniwa 92 tulipata ufaulu wa wastani wa alama 201.6848 na Mwaka
huu 2023 tulikuwa na watahiniwa 71 tumepata ufaulu wa wastani wa alama
237.7887”.
amesema Mwalimu Stella

“Kwa
upande wa mitihani ya upimaji wa darasa la nne kwa Miaka mitatu mfululizo 2020
hadi 2022 tumeweza kufaulisha kwa asilimia Mia moja (100) kwa Miaka yote hiyo
shule yetu imekuwa miongoni mwa shule kumi (10) bora katika Halmashauri ya
Manispaa ya Shinyanga”.
amesema Mwalimu Stella

Amesema kufuatia hatua
hiyo uongozi wa shule ya msingi Lubaga umeanzisha utaratibu wa kutambua na
kuwapongeza wadau wanaochochea maendeleo ya shule hiyo ambapo mkurugenzi wa
kampuni ya Gilitu Interprises Limited amepewa tuzo ya heshima kwa mchango wake
shuleni hapo.

“Kwa
sababu hiyo uongozi uliona umuhimu wa kuweka utamaduni wa kuwatambua na
kuwapongeza wadau wanaoshiriki kuendeleza ustawi wa shule yetu wakiwemo wazazi,
walimu, mashirika mbalimbali, viongozi wa chama na serikali kwa kadri ya nafasi
na uwezo wetu nia ikiwa ni kuendelea kuwatia moyo na kuendeleza ushirikiano
baina yao na shule”.

“Katika
kikao hicho ilibainika umuhimu mkubwa wa kuanza kwa kutambua mchango wa mdau
muhimu sana Bwana Gilitu Makula mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises
Limited ambaye amekuwa na mapenzi makubwa na ustawi wa shule yetu ambaye leo
tunampa tuzo ya heshima kwa moyo wake wa upendo na uzalendo, mdau huyo hasubiri
kuarifiwa wala kuombwa chochote mbali hujitolea muda wake kutembelea shule,
kuongea na walimu na wazazi kupitia kamati ya shule katika maongezi ya kawaida
kisha kubaini uhitaji”.

“Bwana
Gilitu Makula amejitolea kwa moyo kujenga baadhi ya miundombinu yeye mwenyewe
ama kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo kuweka huduma ya umeme shuleni,
kupaka rangi sura ya shule, kuchangia chakula kwa wanafunzi waweze kusoma muda
wa ziada, kuwapatia msaada was are za shule wanafunzi wa kiume wanaotoka kwenye
familia zenye uhitaji na kwa sasa anakamilisha ujenzi wa ofisi ya walimu na
ameahidi kutupatia mashine ya Photocopy ili kurahisisha uzalishaji wa majaribio
kwa wanafunzi”.
amesema Mwalimu Stella

Akizungumza katika hafla
hiyo Mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited Bwana Gilitu Makula
ameshukuru  kupewa tuzo hiyo huku
akiahidi kuendelea kujitolea ili kuchochea maendeleo ya shule hiyo.

Ametumia nafasi hiyo
kuwashukuru Walimu wa shule ya msingi Lubaga kwa ushirikiano wao pamoja na
juhudi wanazozifanya katika ufundishaji ambapo amewaomba kuendelea na juhudi
hiyo ili kuleta matokeo chanya zaidi.

Aidha Bwana Gilitu amesema
amekuwa akipata ushirikiano mzuri kwa walimu wa shule hiyo huku akiipongeza
serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa
kufungua milango wadau kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya
kamati ya shule ya msingi Lubaga Bwana John Myola amesema siri kubwa ya
mafanikio hayo ni ushirikiano uliopo kati ya wazazi, walimu, serikali na wadau
mbalimbali huku akimpongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited
Bwana Gilitu Makula kwa ushiriki wake mzuri katika kutatua changamoto.

Mgeni rasmi  katika hafla hiyo afisa elimu elimu maalum
sekondari Essau Nyeriga ambaye amemwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya
Shinyanga naye amempongeza Mkurugenzi wa kampuni ya Gilitu Interprises Limited
Bwana Gilitu Makula kwa majitoleo yake katika sekta ya elimu ambapo amemuomba
kuendelea na moyo huo wa kuisaidia serikali kufikia malengo yake.

Kwa upande wake Diwani wa
kata ya Lubaga Mhe. Ruben ameomba ushirikiano uliopo uendelea kwa lengo la
kuongeza zaidi ufaulu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Lubaga.

Shule ya msingi Lubaga
iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ni kati ya  shule zilizoshika nafasi ya 10 bora ngazi ya
Halmashauri kwa Miaka minne mfululizo, ambapo hali iliyochangiwa na juhudi na ushirikiano
mzuri baina ya wadau na walimu ambapo hafla 
hiyo imehudhuriwa na wazazi, walimu, watendaji pamoja na wenyeviti wa
mitaa kata ya Lubaga Manispaa ya Shinyanga.