Simanjiro ya kijani yamkuna polepole, amfagilia ole milya




Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi
wa CCM Taifa, Humphrey Polepole akizungumza kwenye kongamano la
Simanjiro ya kijani lililofanyika Mji mdogo wa Mirerani na kuandaliwa na
UVCCM Simanjiro.



Mbunge wa Jimbo la Simanjiro
Mkoani Manyara, James Ole Millya akizungumza kwenye kongamano la
Simanjiro ya kijani lililofanyika Mji mdogo wa Mirerani.




KATIBU wa NEC, Itikadi na
Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole amemfagilia Mbunge wa Jimbo la
Simanjiro Mkoani Manyara James Ole Millya (CCM) kuwa ni mchapakazi na
anayewajibika kwa wananchi.

Hata hivyo, Polepole amewashukia
vikali baadhi ya wanachama na makada wa CCM wanaoiwania nafasi hiyo ili
hali mbunge wa jimbo hilo Ole Millya (CCM) anaendelea na nafasi hiyo.

Polepole ameyasema hayo kwenye
kongamano la Simanjiro ya kijani lililofanyika Kata ya Endiamtu Mji
mdogo wa Mirerani na kuandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM) Wilaya ya Simanjiro.

Amesema Ole Millya ni kijana
mwenye nguvu hivyo viongozi wa CCM na wa serikali wa wilaya ya Simanjiro
wanapaswa kumpa ushirikiano wa kutosha ili wawatumikie wananchi.

“Tumekubaliana kwenye vikao
vikubwa vya chama kuwa mahali palipo na mbunge wa CCM hapaswi kubuguziwa
wala kuguswa na mtu yeyote wala hata wale wa CCM waache unyemelezi,”
alisema Polepole.

Pia, amewakemea vikali baadhi ya
viongozi wa CCM wa wilaya hiyo wenye siasa chafu ambao wanataka
kumkwamisha Ole Millya katika nafasi hiyo.

“Hivi sasa tuna mbunge mmoja jimbo
la Simanjiro naye ni Ole Millya, anapaswa kuachiwa nafasi hiyo kwani
atatekeleza ilani ya CCM kwenye eneo hilo hivyo apewe nafasi afanye kazi
yake,” alisema Polepole.

Amemtaka Ole Millya afanye kazi
yake kwa uadilifu kwa kuwatumikia bila wasiwasi wowote wananchi wa
Simanjiro ambao wana kiu kubwa ya maendeleo.

Alisema Ole Millya ni kiongozi
mzuri anayefanya kazi amekuwa akimshirikisha kwenye baadhi ya changamoto
za wilaya hiyo ikiwemo migogoro ya ardhi hadi anajiuliza kwa nini
hawana umoja.

“Wengine huwa wanaogopa kupigwa
mzinga, sasa wewe tumekuchagua unataka mzinga apigwe nani, hiyo ndiyo
kazi yako ukipigwa mzinga toa, wananchi wako wakikudipu (beep) wapigie
kwani hiyo ndiyo kazi yako kwao unaowaongoza,” alisema Polepole.

Kwa upande wake, James Ole Millya
alimuomba Polepole akemee makundi na mgawanyiko unaofanywa na baadhi ya
viongozi wa CCM wa wilaya hiyo wanaokata majina ya wagombea.

“Simanjiro kuna tatizo kubwa la
baadhi ya viongozi kukata majina ya wagombea kwa sababu hawaungi mkono
au kuwa kwenye kambi yao,” alisema Ole Millya.

Alisema yeye anafanya kazi kwa
moyo mmoja wa kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wala matabaka ila
hafurahishwi na tabia ya baadhi ya viongozi wa CCM kukata majina ya
wagombea.

Alisema hakuna sababu ya kukata
majina ya wagombea wa CCM hasa kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa
ili mradi siyo jambazi au hana sifa mbaya.

Mmoja kati ya wakazi wa wilaya
hiyo, Meshak Laizer alisema maendeleo yaliyopatikana Simanjiro kwa
kipindi cha miaka minne ya ubunge wa Ole Millya ni makubwa sawa na miaka
20.

“Tunaona lami Mirerani, vituo vya
afya vimeboreshwa, hospitali ya wilaya, jengo la utawala la halmashauri
na maji ya mto Ruvu hadi Orkesumet tunamshukuru Rais John Magufuli kwa
kutupatia fedha za maendeleo,” alisema.

Alisema pia mbunge huyo ni
kiunganishi cha wananchi kwani tangu akiwa mbunge kwa tiketi ya Chadema
hakubagua na sasa yupo CCM hana makundi wala kambi.