Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga imekemea na
kulaani vikali ukatili wa kijinsia unaoendelea kwenye jamii Halmashauri ya
Wilaya ya Kishapu huku ikiahidi kuendelea kutetea haki za watoto ikiwemo kutoa
elimu ili waweze kutimiza malengo yao.
Hayo yamebainishwa na katibu wa kampeni
ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga
Bwana Daniel Kapaya pamoja na katibu wa SMAUJATA Wilaya ya Kishapu Bwana James
Onyango Daniel ambapo wamesema ni vyema jamii kuendelea kutoa taarifa za ukatili
ili ziweze kushughulikiwa.
Viongozi hao wamekemea na kulaani vikali
ukatili unaoendelea kufanyika kwenye baadhi ya familia mbapo baadhi ya wazazi
ama walezi huwazuia wanafunzi kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kuhitimu
ikiwa lengo lao wasifaulu watoto wa kike waolewe.
SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga imeahidi
kuendelea kuibua masuala ya ukatili wa kijinsia hasa katika kipindi hiki cha
maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Awali wakizungumza baadhi ya wanafunzi
wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wameeleza kuwa suala la watoto wa
kike wanafunzi kukosa haki yao ya elimu bado linafanywa na baadhi ya
wazazi katika shule za msingi na sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu
Mkoani Shinyanga.
Wanafunzi hao wamesema baadhi ya wazazi
wamekuwa kikwazo kwenye elimu ya watoto wao,wakitaka kuwaozesha ili wapate mali
(Ng’ombe) wakiamini kuwa mali hizo ndiyo nguvu yao ya malezi.
Wamesema moja ya changamoto wanayokutana
nayo wanafunzi wa kike ni kunyimwa mahitaji yao ya msingi ambapo wameiomba
serikali na wadau kuendelea kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia hasa kwa wazazi
na walezi katika Halmashauri hiyo.
Baadhi ya wazazi wa Wilaya ya Kishapu wamekiri
kuwepo kwa changamoto hiyo huku wakiomba serikali na wadau kuendelea kutoa elimu
na kwamba changamoto ya wanafunzi wa kike kupata mimba bado inaendelea katika
shule za msingi na sekondari.
Kwa
upande wake kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa
Polisi Janeth Magomi amewataka wanafunzi, wazazi na jamii kwa ujumla Wilaya ya
Kishapu kushirikiana katika kutokomeza ukatili wa kijinsia ikiwemo kutoa
taarifa za wahalifu kwa wakati ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.TAZAMA PICHA VIONGOZI WA SMAUJATA WAKISHIRIKI KWENYE UZINDUZI WA KAMPENI YA ONGEA NAO KATIKA WILAYA YA KISHAPU.