Tbs yawakabidhi ewura mashine za kutambua kinasaba kwenye mafuta

 

Mkuu
wa Shughuli za Uwekaji Vinasaba (TBS),Mhandisi Florian Batakanwa
akizungumza mara baada ya kukabidhi mashine za kutambua kiasi cha
kinasaba kwenye mafuta hasahasa kwenye soko la ndani ikiwemo Petrol
Station kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) leo
Jijini Dar es Salaam.

Meneja Ufundi idara ya Petrol
(EWURA), Mhandisi Shaban Selemani akizungumza mara baada ya kupokea
mashine za kutambua kiasi cha kinasaba kwenye mafuta hasahasa kwenye
soko la ndani ikiwemo Petrol Station kutoka Shirika la Viwango Tanzania
(TBS) leo Jijini Dar es Salaam.

Moja ya maabara zinayotembea zenye
mashine za kutambua kiasi cha kinasaba kwenye mafuta hasahasa kwenye
soko la ndani ikiwemo Petrol Station ambazo Shirika la Viwango Tanzania
(TBS) limekabidhi kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji
(EWURA) .

**************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
limekabidhi mashine za kutambua kiasi cha kinasaba kwenye mafuta
hasahasa kwenye soko la ndani ikiwemo Petrol Station kwa Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) .

Wamekabidhi maabara zinazotembea
mbili pia na mashine mbili zingine ambazo zitakuwa zinaangalia kama
itatokea katika kufanyakazi kuna mashine ambayo imeharibika watafanya
mabadiliko ili zoezi liweze kuendelea.

Ameyasema hayo leo Mkuu wa Shughuli
za Uwekaji Vinasaba (TBS),Mhandisi Florian Batakanwa akikabidhi mashine
hizo leo Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika makabidhiano
hayo Mhandisi Batakanwa amesema baada ya zoezi hilo kufanyika tayari
kwenye masoko pamoja na kwenye petrol station zote nchini wana magari
kwaajili ya kwenda kufanya utambuzi wa kinasaba.

“Hii itaweza kutusaidia kutambua
mafuta ambayo hayajakidhi ubora au yamechanganywa na mafuta mengine.
Maabara hizi zinatembea na ndani ya gari kuna mashine kwaajili ya
kufanya utambuzi, kuna kompyuta ya kuendesha mashine pamoja na vifaa vya
kuweza kutuonesha maeneo hayo au GPS”. Amesema Mhandisi Batakanwa.

Kwa upande wake Meneja Ufundi idara
ya Petrol (EWURA), Mhandisi Shaban Selemani amesema wataendelea
kuhakikisha mafuta yote yanayosambazwa hapa nchini kukidhi viwango vya
ubora ili kutoharibu magari na mitambo mingine inayotumia mafuta na
vilevile biashara kufanyika kwa uhalali.

“Vifaa hivi ni sehemu ya kutusaidia
tuweze kuendelea kulisimamia zoezi hili ili kuhakikisha mafuta
yanayosambazwa nchini yamekidhi viwango vya ubora unaotakiwa”. Amesema
Mhandisi Selemani.