Tigo yatangaza kuungana rasmi na zantel

Hatua hiyo itasaidia kuboresha zaidi huduma na kukuza sekta ya mawasiliano nchini.
Dar es Salaam. Novemba 4, 2019. Kampuni ya Mawasiliano ya MIC
Tanzania Public Limited Company (Tigo), leo imetangaza rasmi kuungana na
kampuni ya Zanzibar Telecom Public Limited Company (Zantel) baada ya
kukamilika kwa taratibu zote za kisheria na kiumiliki ambapo lengo kuu
ni kukuza na kuboresha huduma za mawasiliano nchini.
Pamoja na kupata vibali kutoka mamlaka zinazohusika, mchakato wa
kuhamisha hisa na umiliki kamili kutoka Zantel kwenda Tigo sasa
umekwisha kamilika. Kufuatia kukamilika kwa zoezi hili sasa makampuni
haya yataunganisha shughuli zake za kiutendaji Tanzania Bara na Visiwani
Zanzibar.
Akizungumza kuhusu muungano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Simon Karikari
alisema hatua hiyo ina manufaa makubwa kwa Taifa; “Ninaamini kuwa
kuunganishwa kwa kampuni hizi – Tigo na Zantel kutajenga huduma jumuishi
kwa watanzania wote siku za usoni. Wateja wote wa Tigo na Zantel
wataweza kufurahia huduma bora kutoka kwenye soko imara litakalosaidia
kuchochea ubunifu kwenye sekta ya mawasiliano,” alisema Karikari. 
Muunganiko wa makampuni haya mawili utasaidia katika kuimarisha utoaji
wa huduma kwa wateja wa Tigo na Zantel waliopo kote Tanzania Bara na
Visiwani. Aidha, muungano huu utawezesha kupanua wigo wa huduma zetu
pamoja na kuongeza ubora wa upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ya
mijini na vijijini. Vile vile muungano huu utasaidia katika usambazaji
wa huduma za mawasiliano kwa makampuni na taasisi mbalimbali nchini na
pia kupanua huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi. 
Tunategemea mafanikio chanya kutokana na muunganiko wa makampuni haya
mawili wenye lengo la kuchangia kwenye maendeleo ya Taifa. 
Zoezi la kuunganisha taratibu za kiutendaji wa makampuni haya mawili
zinatazamiwa kuanza hivi punde. Aidha, wateja wa Tigo na Zantel
wataendelea kupata huduma bila usumbufu wowote kutoka mtandao husika
kwani namba na laini za wateja hazitabadilika.
Tigo
Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo ni kampuni inayoongoza katika utoaji wa
huduma kidigitali hapa nchini.Tigo ilianza kutoa huduma zake mwaka 1995
ikiwa na huduma mbalimbali za sauti, jumbe (SMS), intaneti yenye spidi
pamoja na huduma za kifedha.
Tigo imekuwa mstari wa mbele kuleta mapinduzi ya kidigitali ikiwamo
kuanzisha Smartphone ya Kiswahili, Facebook ya bure, App ya Tigo Pesa na
zaidi kuwa kampuni ya Kwanza kutoa huduma ya kutuma na kupokea pesa
katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.