Ushirika kujali jamii kwa vitendo

 

Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya
Siku ya Ushirika Duniani inayoongozwa na Mwenyekiti Dkt. Gervas Machimu
(wa kwanza kushoto) ikikabidhi mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwa
wauguzi wa Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Maili
Tano wakati wa kuelekea kilele cha Maadhimisho ya siku ya Ushirika
Duniani Julai 3,2021 yanayoendelea Mkoani Tabora

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya
Ushirika nchini Bi. Theresia Chitumbi (kushoto) pamoja na kamati ya
maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani wakikabidhi
mahitaji mbalimbali ya kibinadamu kwa Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete kwa ajili ya kuendeleza utoaji wa huduma
bora hospitalini hapo.

Ushirika umetajwa kuwa nyenzo muhimu
katika kuijali jamii na kuleta ushirikiano mzuri baina ya watu katika
Jamii kwa malengo ya kuhakikisha jamii inauwa na mahusiano mema kwaajili
ya kudumisha na ustawi wa Jamii na hatimaye kuleta matokeo chanya
kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa
Shirikisho la Vyama vya Ushirika Bi. Theresia Chitumbi Julai 01, 2021
wakati akikabidhi mahitaji mbalimbali ya kibinaadamu katika Kituo cha
Afya Maili Tano Halmashauri ya Manispaa ya Tabora akiwa ameambatana na
kamati ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani mkoani
Tabora.

Mwenyekiti Bi.Theresia ameeleza kuwa
kujali Jamii ni miongoni mwa Misingi ya Kimataifa ya Ushirika ambapo
kamati hiyo imetumia fursa ya maadhimisho ya Siku ya Ushirika ambayo
imezinduliwa rasmi Juni 29, 2021 na kilele kufikiwa Julai, 03, 2021
kutekeleza msingi huo wa kujali Jamii. Kamati hiyo imekabidhi mahitaji
ya kibinadamu mbalimbali yakiwemo Sabuni, Sukari, mafuta, miswaki, dawa
za miswaki, taulo za kike vyenye thamani ya Shilling Millioni Mbili.

“Vyama vya Ushirika ni vina majukumu
mengi ikiwemo Kujali Jamii kwani Ushirika unaundwa na Jamii hivyo kuleta
mahitaji haya katika Kituo hiki cha Afya Maili Tano ni sehemu ya
kutimiza wajibu na msingi wa Ushirika tumeona ni vyema kutekeleza hili
hasa tunapoelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani,”
alisema Bi. Theresia

Kamati ikikabidhi mahitaji hayo
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Ushirika
Duniani Dkt. Gervas Machimu nae alieleza kuwa sambamba na makabidhiano
hayo maadhimisho yanaendelea katika Viwanja vya Nanenane Ipuli mkoani
Tabora. Akaongeza kuwa kuwa Kituo hicho cha Afya ni jirani na eneo la
Uwanja hivyo kamati imetekeleza wajibu huo kwa kuzingatia jamii iliyopo
jirani na eneo la Maadhimisho hayo.

Dkt. Machimu aliendelea kwa kutoa
mwaliko kwa wananchi kutembelea mabanda ya maonesho ambapo wadau wengi
wa Sekta ya Ushirika kutoka maeneo mbalimbali wameshiriki pamoja na
shughuli nyingine zinazofanyika uwanjani hapo ikiwa ni pamoja na semina,
makongamano, upimaji wa afya, ushauri wa masuala ya Kilimo, huduma za
kisheria na huduma nyingine nyingi.

Akipokea mahitaji hayo kwa niaba ya
Kituo hicho muuguzi Zaituni Ally ameishukuru kamati hiyo ya Maadhimisho
ya Siku ya Ushirika Duniani na kupongeza hatua iliyochukuliwa kwani
mahitaji hayo yanakwenda kusaidia kuongeza utoaji wa huduma bora kwa
wagonjwa wanaofika katika kituo hicho.

Katika hatua nyingine Kamati hiyo
iliendelea na makabidhiano ya mahitaji ya kibinadamu katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa Kitete mkoani Tabora ambapo Mwenyekiti wa Shirikisho
Theresia Chitumbi pamoja na Kamati ya maandalizi walikabidhi mahitaji
mbalimbali yakiwemo sabuni, mafuta, Sukari, miswaki, dawa za miswaki,
taulo za kike vyenye thamani ya Shillingi Millioni moja na nusu.

Akipokea mahitaji hayo Mganga Mfawidhi
wa Kituo hicho Dkt. Mark Waziri ameishukuru Kamati ya Maandalizi kwa
niaba ya wanaushirika na kutoa wito kwa wadau wa Ushirika kuendelea
kushirikiana na Jamii katika kuboresha na kuendeleza huduma bora za
Jamii zinazonguka maeneo yenye Shughuli za Ushirika kwani kufanya hivyo
kunakuza uhusiano mwema na hatimaye kuongeza tija ya uchumi wa Jamii na
Taifa.