Uvuvi ulivyotumika kichaka cha ujangili ushoroba Kwakuchinja

  • Baadhi ya wavuvi wasiowema hutumia uvuvi kama kazi ya kuzugia wakilenga kufanya ujangili hifadhi

Seif Mangwangi, Manyara

Katika jitihada za kupunguza hatari ya kukamatwa, mshukiwa wa ujangili Maxi Mirumbe alisimama kidogo katikati ya pori Aprili 4 mwaka huu 2024 ili kupunguza ukubwa wa mzigo baada ya kukimbizana na askari wa wanyamapori waliomkuta hifadhini. 

Mtuhumiwa wa ujangili wa nyama ya swala pala Maxi Mirumbe akiwa amebeba nyamapori katika Toyo baada ya kunaswa na Maaskari wa Juhibu na Tawa akiisafirisha kuelekea Babati, Mkoani Manyara

Hata hivyo, haikuchukua muda, maofisa wa uhifadhi walikuwa wameshamkaribia dereva huyo wa bodaboda anayetuhumiwa kubeba nyamapori ya swala katika pikipiki yake na kumkamata kwa ajili ya kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.

Kukamatwa kwa Mirumbe ni matokeo ya ushirikishwaji wa kina wa wananchi katika kulinda rasilimali zao. Serikali pamoja na wadau wa uhifadhi, sekta binafsi, wananchi na asasi za kiraia wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa zinazosaidia kutiwa mbaroni kwa baadhi ya majangili. 

Mirumbe na bodaboda yake yenye usajili wa namba MC 744EDY aina ya Kinglion alinaswa na maaskari wa Mamlaka ya usimamizi wanyamapori (TAWA), wakishirikiana na askari wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge (JUHIBU) maarufu kama VGS baada ya kupata taarifa za siri kutoka kwa wananchi.

Mtuhumiwa wa ujangili Maxi Mirumbe akiwa amenaswa na maaskari wa wanyamapori wa Jumuiya ya hifadhi ya Burunge (JUHIBU), na Tawa akiwa katika harakati za kusafirisha Nyama ya Swala pala baada ya kuua wanyama hao zaidi ya sita katika pori la Jumuiya hiyo

Abubakar Hatibu Msuya, Mwenyekiti wa kijiji cha Vilimavitatu pamoja na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge, Benson Mwaise wanasema mtandao wa utoaji wa taarifa za siri miongoni mwa wananchi  ndio uliosaidia kukamatwa kwa Maxi licha ya wenzake wawili aliokuwa nao katika ujangili huo kukimbia.

“Nikiwa nimelala saa11 alfajiri nilipata taarifa ya kukamatwa kwa majangili wa swala ambao walikuwa wameua swala sita aina ya pala na kuwabeba kwenye ndoo, askari wetu wa VGS na TAWA walikuwa wakiwakimbiza baada ya kuona pikipiki yake haikimbii akasimama kukata kamba kupunguza sehemu ya mzigo ndipo aliponaswa,” anasema Msuya. 

Ushoroba ya Kwakuchinja unapatikana katikati ya hifadhi mbili za Taifa  ya  Ziwa Manyara na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Katika wilaya za Babati Mkoani Manyara na Monduli Mkoani Arusha ikiwa ni mapitio ya asili ya wanyamapori kwa ajili kuzaliana, kutafuta chakula na hata makazi kwa baadhi yao.

Mfumo wa ushirikiano wa utoaji wa taarifa za siri kuhusu matukio ya ujangili uliotengenezwa na vijiji vinavyozunguka ushoroba wa Kwakuchinja hasa vile vilivyopo kwenye ushirikiano wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge (JUHIBU), umekuwa ukisaidia kudhibiti matukio ya ujangili katika ushoroba wa Kwakuchinja na kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu kama Mirumbe.

Ujangili wa viumbepori ni tishio kubwa kwa uhai wa ushoroba wa Kwakuchinja ambao umekuwa kielelezo cha mfano nchini kutokana na hatua mbalimbali zinazotumika kulinda bioanuai yake.

Uvuvi watumika kichaka cha ujangili

Pamoja na jitihada mbalimbali za kudhibiti majangili ambao wamekuwa wakiua wanyamapori na kuchoma mkaa, baadhi ya majangili wamekuwa wakitumia kazi za uvuvi wa samaki katika Ziwa Manyara kama njia ya kificho cha kufanyia ujangili, jambo ambalo ni vigumu kubainika pindi wanaposakwa na vyombo vya usalama.

Kuendelezwa kwa ujangili wa kinyemela ambao umezidi kupungua miaka ya hivi karibuni katika eneo hilo, kunatisha ushoroba huo ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya vijiji 10 vinavyounda ushoroba huo. 

wavuvi wakiwa pembezoni mwa ziwa manyara wakisubiri muda wa kuingia ziwani kwaajili ya kufanya uvuvi

Mbali ya taarifa za siri kufanikisha kukamatwa kwa Mirumbe, Aprili 22, 2023 ushirikiano huo huo ulifanikisha kukamatwa kwa jangili Bernard Mtinange maarufu kama Meja aliyekuwa ameua Twiga tayari kwa kuanza kuuza kitoweo chake. Bernard hivi sasa ni mfungwa baada ya kutiwa hatiani. 

Matukio haya yanawakilisha changamoto kubwa katika uhifadhi wa wanyamapori na juhudi za kukabiliana na biashara haramu ya nyama ya wanyamapori katika ukanda wa ushoroba wa Kwakuchinja.

Kukamatwa kwa Maxi na Meja kunadhihirisha jinsi biashara haramu ya wanyamapori inavyofanyika wakati wowote, hata mchana au asubuhi. Majangili wamekuwa wakiuza nyamapori kwa bei ndogo tofauti na nyama ya ng’ombe, mbuzi au kondoo ambazo bei zake zimekuwa kubwa huku wananchi wa kawaida wakishindwa kuzimudu. Hali hii inaelezwa ni sababu mojawapi ambayo imekuwa ikichochea uwindaji haramu. 

Takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonyesha kuwa kabla ya Septemba 25, 2020 Nyati alikuwa akiuzwa shilingi Milioni 4.1, huku swala pala akiuzwa Shilingi laki tatu (300,000). Hata hivyo Serikali kupitia kwa aliyekuwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Aloyce Nzuki ilitangaza kushusha gharama hizo kwa watu waliokuwa na nia ya kutaka kufuga wanyamapori ambapo Nyati aliuzwa kwa bei ya 210,000 na swala pala aliuzwa kwa bei ya elfu 90.

‘Mchana wavuvi, usiku majangili’

Hatibu Msuya Mwenyekiti wa kijiji cha Vilimavitatu anasema kumekuwepo na taarifa za majangili kutumia uvuvi kama sehemu ya wao kujificha nyakati za mchana na nyakati za usiku huingia hifadhini kuua wanyamapori.

Anasema Bernard Meja ambaye hivi sasa ni mfungwa ni miongoni mwa majangili aliyekuwa akijihusisha na shughuli ya uvuvi katika Ziwa Manyara ambaye alitiwa mbaroni na askari wa wanyamapori wanaolinda hifadhi ya Jumuiya ya Burunge WMA, akiwa ndani ya hifadhi ya Jumuiya ya Burunge ameua twiga ndani ya eneo hilo lililohifadhiwa. 

Amos Bernard Mtinange maarufu kama Meja ambaye amekuwa akifanya shughuli za uwindaji haramu nyakati za usiku huku mchana akionekana ziwani akiendelea na shughuli za uvuvi wa samaki alikabiliwa na adhabu kali  ya kifungo cha miaka 23 jela kutokana na kosa alilokutwa nalo. 

Watu kama Amos wanaelezwa kuwepo wengi katika eneo la ushoroba wa Kwakuchinja ambao wamekuwa wakitumia ajira ya uvuvi kama kichaka cha kujificha wasiweze kujulikana hufanya shughuli gani nyingine lakini taarifa za awali zinabainisha kuwa wamekuwa wakijishughulisha na ujangili wa viumbepori ikiwemo uuaji wa wanyamapori nyakati za usiku. 

Kuwepo kwa genge la majangili inawezekana kusababishwa na taratibu zisizoeleweka kwa watu wanaojishughulisha na uvuvi katika Ziwa Manyara kufuatia wengi wao kufanya shughuli hiyo pasipokuwa na vibali maalum vinavyowatambulisha kama wavuvi katika eneo hilo zaidi ya kulipa ushuru kwa Mamlaka ya Serikali ya Halmashauri ya Babati inayosimamia eneo hilo pindi wanapomaliza kazi ya kuvua. 

Afisa uvuvi Wilaya ya Babati Haji Deusi anakiri kuwa hapo awali taratibu za uvuvi katika ziwa Manyara zilikuwa hazieleweki kutokana na eneo hilo kuvamiwa na watu wengi hali iliyolazimu kuanzisha chombo kitakachoendeshwa na wavuvi wenyewe kinachojulikana kama Beach Management Unit (BMW).

Kina Mama katika ziwa Manyara wakitengeneza samaki walizonunua kutoka kwa wavuvi tayari kwenda sokoni. Baadhi ya wavuvi wamekuwa wakitumia uvuvi kama sehemu ya kujificha mchana, usiku huingia hifadhini na kufanya ujangili

Anasema katika kudhibiti uvuvi haramu ndani ya ziwa hilo na kuweka eneo hilo salama dhidi ya ujangili wa aina yoyote ile, wilaya iliamua kuondoa wavuvi katika eneo la forodha ya Maramboi na kuliacha eneo hilo kwa ajili ya uhifadhi na wavuvi kuwahamishia eneo la Mfulang’ombe.

Anasema pia kumekuwa na ukaguzi wa mara kwa mara wa pamoja kwa ushirikiano wa kamati ya uhifadhi ziwani (Beach Management Unit), askari wa  uvuvi, askari wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge, mwekezaji kampuni ya Chemchem  pamoja na askari wa TAWA lengo ni kubaini shughuli zinazoendelea mbali ya uvuvi wa samaki katika eneo hilo. 

“Baada ya kufanikiwa kuhamisha watu kutoka eneo la Maramboi ambalo lilikuwa na wanyamapori wengi wanaofika ziwani na kuwa katika hatari ya kuuawa na wavuvi, hali ya ujangili iliweza kupungua sana. Hata hivyo katika doria zetu mwaka 2022 tulifanikiwa kumnasa Mama ntilie mmoja akiwa amebeba nyamapori katika eneo la ziwani,” anasema Deusi.

“Operesheni hizi zilifanikiwa sana kunasa wahalifu ambapo tangu tumeanza tumeshakamata majangili ikiwemo mvuvi mmoja aliyekuwa akiwinda bata maji katika eneo la Kisese, mama mmoja katika eneo la Mbuyuni akiwa amebeba nyamapori, Minjingu tulikamata mwingine akiwa kabeba nyama ya swala na hili la Bernard akiwa ameua twiga,” anasema.

Vitendea kazi vya doria bado mtihani

Hata hivyo, anasema zoezi la ulinzi ni mgumu sana kutokana na kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha hususani boti ya kuwawezesha kuingia ndani ya ziwa na kufanya ukaguzi wa kina ili kuweza kubaini wahalifu ambao wengi wao wamekuwa wakikimbilia katikati ya ziwa mara baada ya kuhisi kubainika kutafutwa.

Ili kukabiliana na ujangili, wadau wa uhifadhi wakiwemo Chemchem Association wanaotekeleza mradi unaofadhiliwa na mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili wamekuwa wakishirikiana na Serikali kufanya doria ili kuwakamata majangili katika ushoroba huo wa Kwakuchinja ambao huvutia pia watalii kutazama wanyamapori waliopo. 

Afisa tawala wa taasisi ya Chemchem kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Ernest Elia anasema taasisi hiyo imekuwa ikifanyakazi na wadau wengine wa hifadhi katika eneo hilo kuhakikisha ushoroba wa Kwakuchinja unakuwa salama wakati wote.

“Tumekuwa na kikosi cha pamoja cha doria kuzuia ujangili pamoja na uvuvi haramu katika eneo lote la Ziwa Manyara, pia tumekuwa tukifuatilia wanyama wote katika eneo la ushoroba wa Kwakuchinja na zaidi tumekuwa na mradi wa kutoa elimu ya uhifadhi kwa wanafunzi katika shule za sekondari zinazozunguka eneo lote la shoroba,” anasema Elia.

Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Tangwe amesema kupitia vikao vya mara kwa mara vya ujirani mwema na vijiji vinavyozunguka hifadhi za Tarangire, Manyara na eneo lote la ushoroba wa Kwakuchinja wamefanikiwa kudhibiti vitendo vya ujangili.

Ili kudhibiti ujangili, amesema ndani ya kamati ya ulinzi na usalama amewajumuisha wakuu wa hifadhi za Tangire, Manyara, Tawa na viongozi wa Juhibu kwa lengo la kuhakikisha wanaungana kuweza kudhibiti ujangili katika wilaya ya Babati.

Kwakuchinja ni miongoni mwa shoroba chache zilizosalia katika ukanda wa mikoa ya kanda ya Kaskazini ambayo inaelezwa bila jitihada za makusudi kuchukuliwa inaweza kutoweka kama ilivyokuwa kwa shoroba nyingine nchini. Tanzania ina shoroba zisizopungua 60 ambazo ni mapito ya asili ya wanyamapori kutoka hifadhi moja kwenda nyingine kusaka malisho, kuzalisha au makazi. 

Ucheleweshaji fedha kikwazo vita ya ujangili

Ili taarifa za wananchi zizae matunda, askari wa uhifadhi wa maeneo hayo ya ushoroba wakiwemo wa Juhibu wanahitaji usafiri wa haraka na gharama nyingine za kiuendeshaji ili kuwa na doria imara zinazozaa matunda. 

Hata hivyo, Mwaise anasema ucheleweshwaji wa gawio la fedha kutoka Serikali kuu limekuwa likidhoofisha jitihada za kulinda eneo hilo kufuatia kukwama fedha za kuwekea mafuta magari ya kufanyia doria pamoja na kucheleshwa kwa posho za askari wanaolinda na posho kwa watoa taarifa za siri.

Takwimu za ujangili

Kauli hii inaungwa mkono na kamati ya kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii kupitia katika taarifa yake ya kamati kwa Bunge kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2023/24 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2024/2025.

Katika taarifa yake, kamati hiyo imekiri kuwepo kwa ucheleweshaji wa mgao wa fedha za wanufaika kuwafikia kwa wakati na kwamba hali hiyo inasababisha kukosekana kwa fedha za uendeshaji wa ofisi, ulinzi wa rasilimali za wanyamapori, na kudhoofisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo vijijini. 

“Hali hii inahatarisha ustawi wa uhifadhi katika maeneo ya Jumuiya hizi ambapo vitendo vya ujangili wa wanyama vinaongezeka na kushindwa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Januari, 2024, jumla ya madai ya fedha za wanufaika (WMAs 13, Vijiji 50, Halmashauri za Wilaya 29) zilizowasilishwa Wizara ya Fedha ni zaidi ya  Shilingi Bilioni 8.01.  Hata hivyo, hadi kufikia Februari, 2024, Serikali ilikuwa imelipa zaidi Shilingi bilioni 1.4  tu ikiwa ni mgao wa mwezi Julai, 2023.

Ripoti hii maalum ni sehemu ya mafunzo ya uandishi wa habari za bioanuai yaliyofadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) chini ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.