Uyui kulima hekta 5,000 za pamba msimu huu

************************************
WAKAZI wa Halmashauri ya
Wilaya ya Tabora(Uyui) wanatarajia kulima hekta 5,000 za zao la pamba
katika msimu wa kilimo unaoendelea mkoani Tabora.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Mkuu
wa Wilaya ya Uyui Gift Msuya wakati akitoa taarifa ya kilimo cha zao
hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora alipotembelea Wilaya hiyo kuhamasisha
shughuli za kilimo.
Alisema kutokana na makadirio hayo wanatarajia kuzalisha tani 3,500 za zao hilo katika mavuno yajayo.
Msuya alisema jumla ya vyama msingi nane vimeshapokea mbegu na ugawaji kwa wakulima mbalimbali unaendelea.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema katika
msimu uliopita walilenga kulima hekta 4,000 lakini walifanikiwa kulima
hekta 1,700 na kuwafanikiwa kuzalisha kilo milioni 1.2.
Alisema katika kilo hizo wakulima walipwa shilingi milioni 1.5 ambapo wakulima wameshalipwa na Kampuni ya KCCL na KOM.
Aidha alisema hadi hivi sasa Vyama vya Msingi vinadaiwa shilingi milioni 53.4 ikiwa ni gharama za mbegu na pembejeo.
Msuya alisema wamewaagiza
Watendaji wa Vijiji kushirikiana na Askari wa Akiba kuhakikisha
wanawabaini wale wote ambao wamechukua pembejeo na hawakulima na wale
waliotorosha pamba yao ili waweze kulipa madeni yao.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa
Tabora Aggrey Mwanri aliwaagiza viongozi mbalimbali wa kuanzia ngazi ya
Kijiji hadi Kata kulima kitaalamu ekari tatu za pamba ili kuwahamasisha
wananchi wengi kushiriki katika kilimo hicho.
Alisema hatua hiyo itaisaidia
Halmashauri yao kupata ushuru mwingi unaotokana na mauzo ya pamba ikiwa
ni sehemu ya kuongeza mapato yake ya ndani