Wafanyakazi wanne wa kampuni ya uwindaji ya green miles wakamatwa na polisi

Wafanyakazi
wanne wa kampuni ya uwindaji ya Green Miles iliyoondolewa katika kitalu
cha Lake Natron(east) wilayani Longido wanashikiliwa na polisi kwa
madai ya kukaidi agizo la Serikali  kuondoka wa hiari katika kitalu
hicho.


Wafanyakazi
hao wamekamatwa na polisi leo Jumatano Januari 22, 2020 waliokuwa
wameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Longodo mkoani
Arusha.

Wanatuhumiwa kuendelea na kazi katika kitalu hicho licha ya kutakiwa kuondoka Januari 20, 2020.

Katibu
tawala Wilaya ya Longido, Toba Nguvila amesema baada ya wafanyakazi hao
kukamatwa, eneo hilo litakuwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) kwa kushirikiana na polisi.

Ofisa
wanyamapori wa kikosi cha kuzuia ujangili Mkoa wa Arusha, Emmanuel Pius
amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni kaimu meneja wa kambi ya Tandala,
Lazaro Lembrise, Moses Sikange, Mohamed Bembe na  Hassan Mahonza.