Waitara aomba wananchi kuchagua viongozi wenye hofu ya mungu

Image result for Naibu waziri waitara
 
 
Na Paschal Dotto-MAELEZO.

Katika
kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika nchi nzima
Novemba 24, 2019, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Mhe. Mwita Waitara amewaomba viongozi wa Dini kuwahamsisha
wananchi kuchagua viongozi wenye hofu ya Mungu.

Akizungumza katika Mkutano wa Kujadili namna Taasisi za Dini
zinzvyochangia Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda uliofanyika katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Mhe.
Waitara amesema kuwa ni muhimu kuwachagua viongozi wenye hofu ya Mungu
na waadilifu kwa wananchi ili kuiunganisha Serikali katika kuleta
maendeleo kwa wananchi.
“Viongozi wa Dini nyie mnahubiri amani na haki, watu wakipata haki maana
yake nchi inatulia, kwa hiyo hakikisheni mnawahubiria watu wenu kuhusu
kuchagua viongozi walio na hofu ya Mungu ambao pia ni waadilifu kwa
wananchi ili kuondoa migogoro mbalimbali ambayo imekuwa ikisababishwa na
viongozi wala rushwa kwenye mitaa yetu ikiwemo ile ya ardhi”, ameeleza
Mhe.Waitara.
Waziri Waitara alisema kuwa viongozi waadilifu huwa wanawajibika bila
shida yeyote, kwa hiyo ni muhimu kuunganisha juhudi za Mhe. Rais John
Pombe Magufuli kwa wananchi kwani uwajibikaji wake ni mkubwa katika
kuwaletea maendeleo wananchi.
Alianisha sifa nzuri za kiongozi kuwa ni yule mwenye maono, maamuzi
sahihi, anayesimamia maono na maamuzi yake, sifa ambazo Rais Magufuli
anazo, kwa hiyo ili kuendelea kuleta maendeleo ni lazima viongozi wa
Serikali za Mitaa ambako maendeleo yaanzia wawe waadilifu na wenye hofu
ya mungu.
Waziri Waitara alisema kuwa mpaka Oktoba 17, 2019 wananchi milioni
19,686,000 walikuwa wamejiandikisha, sawa na asilimia 86 ikilinganishwa
na mwaka 2014 ambapo wananchi Milioni 11 walijiandikisha sawa na
asilimia 63.
Aidha Waitara alisema kuwa katika hatua za uchaguzi huo wagombea
wataanza kuchukua fomu za kugombea kuanzia oktoba 29, 2019 na kwamba
itakapofika Novemba 5, 2019 wasimamizi wa Uchaguzi watabadika majina ya
wagombea kwa hiyo viongozi wa dini wanatakiwa kuwasaidia wananchi kujua
kiongozi mwadilifu na pia kusali kwa ajili ya kupata kiongozi bora
katika mitaa mbalimbali nchini.
Waziri Waitara alisema kuanzia Novemba 17 hadi 23, 2019, itakuwa ni muda
wa kampeni ambapo amewataka wagombea kuomba kura kwa kujenga hoja kwa
wananchi na kuwataka Wakuu wa Mikoa na Viongozi wa Dini kusimamia
kikamilifu suala ya amani wakati wa kampeni.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kuwa
watu wanatakiwa kubadilika na kufuata kasi ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na wasaidizi wake kwani wanakimbizana kuwaletea
maendeleo wananchi.
“Kuna watu bado hajabadilika na hawataki kubadilika, lakini ukiangalia
makusudi ya Rais wetu, Makamu wake, Waziri Mkuu na Mawaziri
wanakimbizana kuleta matokeo kwa wananchi, lakini huku chini ni shida
kidogo, kwa hiyo nawaomba viongozi wetu wa Dini tuwahamasishe wananchi
wetu Novemba 24, 2019 wajitokeze kuwachagua Wenyeviti wa Serikali za
Mitaa wenye hofu ya Mungu”, alieleza Makonda.