Na, Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.
Vijana wanaofanya bisashara kubwa na ndogo Jijini Arusha wameahidi kulipa kodi ipasavyo na kusajiri biashara zao, baada ya kupata elimu ya masuala ya kodi kutoka kwa wataalam, yaliyowezeshwa na Shirika lisilo la serikali la Okoa New Generation.
Wakizungumza katika mdahalo uliojumuisha takriban vijana 50, wameeleza namna walivyonufaika na elimu hiyo, na kuwapa mwanga wa kutambua haki na wajibu wao katika masuala ya kulipa kodi.
Aidha wamebainisha namna ambavyo wamekuwa wakifuatwa na Watendaji wa TRA katika biashara zao, kukadiriwa mapato kabla ya kuanza biashara sambamba na kudaiwa kodi kwa wale wenye mapato chini ya shilingi milioni nne kwa mwaka, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
“Elimu hii imeleta mwanga mkubwa kwetu, ni dhahiri tulikuwa tunalipa kodi kama adhabu ingawa ni wajibu wetu, hii ilitokana na ukosefu wa elimu, ya kutosha, ushauri na ushirikiano kati yetu vijana na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), tunatamani elimu hii iwe endelevu ili iwafikie vijana wengi wanaofanya biashara”
“Lakini pia tunawaomba Afisa Maendeleo ya Jamii kuwajibika kwa nafasi zao, watoke ofisini na kuwafuata vijana mitaani kuwapa ushauri, kuwaeleza namna ya upatikanaji mikopo iliyopo katika halmashauri, elimu ya mikopo na faida za kuunda vikundi” wamebainisha Pialla Silayo, Steven Joaeph, na Shedrack Pesambili.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngarenaro na Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii Jiji la Arusha Issaya Doita amewataka Madiwani kuwasimamia kikamilifu watendaji katika kata ili kwenda kutoa elimu ya mikopo na aina za kodi kwa wananchi badala ya kukaa ofisini.
“Kipekee nalipongeza shirika la Okoa New Generation kwa elimu hii muhimu kwa vijana, iliyowapa nafasi ya kuwakutanisha kuibua changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi, hatua hii inaleta matumaini ya kuwa na vijana wanaojitambua katika masuala ya kodi na fulsa za mikopo zilizopo katika halmashauri yetu, na habari njema ni kwamba serikali imetenga shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya wajasiriamali, hivyo zichangamkieni zipo kwa ajili yenu” amefafanua Doita.
Pia amewashauri Watendaji wa TRA wanaotoa elimu kwa wateja, kuwatembelea Watendaji katika Kata na Mitaa kuwaelimisha, ili watendaji hao watakapokuwa katika majukwaa na mikutano wawaelimishe wananchi wao kuhusu masuala ya kodi.
Vile vile Mratibu wa mradi wa shiriki na shirikishwa kulipa kodi kutoka shirika la Okoa New Generation Shaban James amesema elimu ya kodi kwa vijana itakuwa endelevu ili kuongeza idadi ya walipa kodi kutoka watu milioni mbili iliyopo hivisasa.
Ameongeza kuwa, kipaumbele cha elimu hiyo ni kuhamasisha ulipaji kodi na kusajiri biashara zao, kuwakumbusha viongozi wajibu wao, na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa muhimu zinazohusiana na biashara zao.
“Kwa ushirikiano na Shirika la Restless Development tutaendelea kutoa elimu kwa vijana, lengo ni kuona idadi kubwa inajitambua na kuwa na uelewa mkubwa katika masuala ya ulipaji kodi ili kulingizia taifa mapato” amesema Shaban.
Hata hivyo Mtendaji kutoka kitengo cha mtoa elimu kwa mteja (TRA) Nicodemus Massawe amesema kulipa kodi ni wajibu wa kila mtu anayefanya shughuli za kiuchumi, huku mwenye mapato ya kuanzia milioni 11 kwa mwaka kuwa na mashine ya kutolea risiti ya (EFD).
Amefafanua kuwa licha ya kukusanya mapato pia wanawashauri na kuwapa elimu wafanyabiashara ili badala ya kuifunga , waadilishe eneo au aina ya biashara ya awali.
“Kazi yetu ni kukadiria, kukasimu na kukusanya mapato kuyapeleka serikalini ili kutekeleza miradi mbalimbali, na nchi yoyote haiwezi kwenda bila kodi, tunakusanya zaidi ya asilimia 50 ya mapato yanayotakiwa, hivyo tutaendelea kutoa elimu kwa makundi yote na kila mmoja nayefanya shughuli za uchumi, ahakikishe anapata namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN)” ameeleza Massawe.
*********************