Msajili wa Baraza la Veterinari
Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli akisisitiza jambo wakati wa kikao
kilichojadili kuhusu changamoto zinazohusu tasnia ya Mifugo kwenye
uuzaji na udhibiti wa madawa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa
Ofisi ya Baraza la Veterinari Temeke Mkoani Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa kikao
kilichoitishwa na Baraza la Veterinari kilichojadili kuhusu changamoto
zinazohusu tasnia ya Mifugo kwenye uuzaji na udhibiti wa dawa feki
wakisikiliza hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa zinazohusu tasnia
ya Mifugo kwenye uuzaji na udhibiti wa madawa. Kikao hicho kimefanyika
katika ukumbi wa Ofisi ya Baraza la Veterinari Temeke Mkoani Dar. es
Salaam.
Mwenyekiti wa kikao ambaye pia ni
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya MULTIVET, Dkt. Henry Ruhinguka
akihitimisha kikao kilichoitishwa na Baraza la Veterinari Tanzania
kilichojadili kuhusu changamoto zinazohusu tasnia ya Mifugo kwenye
uuzaji na udhibiti wa madawa. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa
Ofisi ya Baraza la Veterinari Temeke Mkoani Dar es Salaam.
Wauzaji na wasambazaji wa madawa ya
mifugo wametakiwa kuzingatia utaratibu ambao umewekwa na Serikali
kupitia Baraza la Veterinari Tanzania ili kutoa huduma stahiki kwa
wafugaji.
Hayo yalisemwa na Msajili wa Baraza la
Veterinari Tanzania, Dkt. Bedan Masuruli wakati wa kikao na wauzaji na
wasambazaji wa dawa kilichojadili kuhusu changamoto zinazohusu tasnia ya
Mifugo kwenye uuzaji na udhibiti wa madawa kilichofanyika Jijini Dar es
Salaam Mei 19, 2021.
Dkt. Masuruli alisema kuwa bado lipo
tatizo kwa baadhi ya wauzaji na wasambazaji wa madawa hayo kutozingatia
taratibu ambazo zimewekwa na hivyo kusababisha madhara kwa wafugaji kwa
kutopata huduma stahiki.
Aliongeza kuwa wauzaji na wasambazaji
wa madawa hayo wanatakiwa kufuata na kuzingatia utaratibu uliowekwa kwa
kuhakikisha madawa yote ya mifugo yanauzwa sehemu ambayo ni sahihi na
imesajiliwa na kutambulika na Baraza la Veterinari Tanzania.
Aidha, Dkt. Masuruli aliwahimiza
wamiliki hao kuwatumia wataalam wa mifugo katika kutoa huduma hizo kwani
kwa kutofanya hivyo kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa wafugaji
na hatua zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu
zilizowekwa.
Dkt. Masuruli aliendelea kusema kuwa
Baraza litaendelea kuwaelimisha wauzaji na wasambazaji wa madawa ya
mifugo ili waweze kujua sheria, kanuni na taratibu ili waweze kutoa tiba
stahiki kwa wafugaji pale wanapohitaji huduma hiyo.
Katika kikao hicho wauzaji na
wasambazaji wamekubaliana kwa pamoja kudhibiti uingizwaji na usambazaji
wa madawa feki ambayo yamekuwa yakitumiwa na wafugaji kwa kutokujua na
kusababisha mifugo yao kutopona na mfugaji kudhoofika kiuchumu.
Naye Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye
pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya MULTIVET, Dkt. Henry Ruhinguka
alisema lipo tatizo la dawa hizo kuuzwa maeneo ya wazi kama minadani
ambayo sio sahihi kisheria.
Dkt. Ruhinguka alitumia fursa hiyo
kuwahimiza wauzaji na wasambazaji wa madawa hapa nchini kushirikiana na
serikali kuhakikisha wanadhibiti tatizo la madawa kuuzwa bila utaratibu
unaotakiwa na kuhakikisha wanawadhibiti watu wanaoingiza madawa feki
yanayokuja kuleta matatizo kwa wafugaji na kuwarudisha nyuma kiuchumi.