Washtakiwa watano wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akiwemo tenga wamwandikia barua dpp kuomba kukiri makosa yao

Washtakiwa
watano wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akiwemo wakili, Dk Ringo
Tenga wamemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP)
kuomba kukiri makosa yao.



Wakili
wa washtakiwa hao, Byrson Shayo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu leo Ijumaa Septemba 27, 2019 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili
ya kutajwa.

Dk
Tenga ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni ya mawasiliano ya
Six Telecoms Limited na wenzake, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi
namba 73/2019.


Washtakiwa hao  wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo la kutakatisha
fedha na kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) hasara ya
Dola za Marekani 3,748,751.


Mbali
na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte
ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Mfanyabiashara na Mkurugenzi
wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha
na Kampuni ya Six Telecoms.

Wakili
Shayo amedai  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa
wamejadiliana na wateja wao na baada ya majadiliano hayo wameamua
kumuandikia DPP barua kwa kuzingatia maagizo ya Rais John Magufuli
aliyoyatoa Septemba 22,  2019.


Amesema
kutokana na uamuzi huo, wanaiomba mahakama kutoa ahirisho la siku 14
kuanzia leo ili waweze kupata  majibu ya barua hiyo.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo
hadi Oktoba 11, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande