Wataalam wa ndani wanaotekeleza miradi ya maji nchini waelekezwa kushirikiana

 

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (mbele) akielekea kwenye mradi wa maji Busokelo, Mkoani Mbeya.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amkitua ndoo kichwani Mama Jenister wakati wa ziara yake kwenye mradi wa Iziwa, Mbeya Vijijini.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akijiridhisha na huduma ya maji kwenye mradi wa Iziwa, Mbeya Vijijini. Kushoto ni Meneja wa Wakala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoani Mbeya, Mhandisi Mathayo Athuman

Na Mohamed Saif

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ameridhishwa na ushirikiano wa ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa na wataalam wa ndani (force account) kwenye Mkoa wa Mbeya na amezitaka mamlaka za maji zingine kote nchini kuiga mfano huo.

Amesema na kuelekeza hayo Agosti 6, 2020 Wilayani Rungwe alipohitimisha ziara yake ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji inayotekelezwa kwa ushirikiano wa wataalam wa ndani kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWASA), Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mbeya na Bodi ya Bonde la Ziwa Rukwa.

“Ninahitaji kuona taasisi za maji zikishirikiana, mnapaswa kutambua kwamba mnatekeleza majukumu yenu kwa niaba ya wizara hivyo basi, taasisi zote zinapaswa kuelewa kwamba lengo letu ni moja nalo si lingine bali ni kuwafikishia huduma ya maji wananchi,” alisema Mhandidi Sanga.

Awali, katika taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mbeya UWASA, Mhandisi Ndele Mengo ilielezwa kuwa jumla ya miradi nane inatekelezwa mkoani humo kwa mfumo wa force account mingine ikiwa ni baada ya wakandarasi waliyokuwa wakiijenga kushindwa kuikamilisha kwa wakati na hivyo kusitishiwa mikataba na Wizara.

Mhandisi Mengo aliitaja miradi inayotekelezwa mkoani humo kwa mfumo wa force account kuwa ni mradi wa Bulongwe, Busokelo, Vwawa-Mlowo, Chitete, Shongo-Mbalizi, Ndalambo, Chunya na Kingili-Kapapa.

Katibu Mkuu Sanga alifurahishwa na hali aliyoikuta kwenye miradi inayotekelezwa na wataalam hao na alielekeza mamlaka za maji zingine kote nchini zijifunze ujenzi bora wa miradi kwa mfumo huo wa force account kutoka kwa wataalam wa Mbeya.

“Nimefurahishwa na namna mlivyoshirikiana kwa pamoja kujenga hii miradi niliyoitembelea, nimefarijika zaidi kuona tayari wananchi wameanza kupata huduma ya maji kama ambavyo mara zote Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli anavyotuelekeza,” alisema Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alisema Mbeya imedhihirisha kwamba miradi ya maji kujengwa kwa ushirikiano wa wataalam wa ndani inawezekana na alienda mbali zaidi kwa kutaja faida zilizopatikana kwa kutumia wataalam wa ndani kujenga miradi kwa namna aliyoishuhudia kwenye ziara yake mkoani humo.

“Mfumo wa force account unazo faida nyingi sana, lakini kwa uchache kama nilivyoshuhudia hapa ni kwamba unawezesha wananchi kuwahi kupata maji yaani inakamilika kwa wakati lakini pia gharama ya ujenzi wake ni nafuu ikilinganishwa na baadhi ya miradi ya wakandarasi,” alisema Mhandisi Sanga.

Aidha, aliwaelekeza wataalam wote wa ndani wanaohusika na ujenzi wa miradi kwa mfumo huo wa ushirikiano kuhakikisha wanazingatia ubora wa ujenzi ili kuhakikisha inakuwa endelevu.

“Maelekezo wangu kwa wataalam wetu waliokabidhiwa miradi ni kuhakikisha tunakuwa na miradi endelevu; msikimbilie tu kujenga ni lazima mzingatie suala la viwango wakati wote wa ujenzi ili miradi hiyo idumu kwa muda mrefu zaidi na thamani ya fedha iliyotumika ni lazima ionekane,” alielekeza Katibu Mkuu Sanga

Mhandisi Sanga alisema dhamira ya Serikali ni kuwa na miradi endelevu na kwamba wataalam watakaojenga miradi ambayo haitodumu hawatovumiliwa.

“Hatujengi miradi ili itoe maji kwa kipindi kifupi, tunajenga miradi itakayohudumia hata vizazi vijavyo; tunataka hata baada ya miaka 20 miradi iwe inatoa maji,” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Ziara hii ya Mhandisi Sanga kwenye Mikoa ya Mbeya na Songwe ni ya pili tangu ateuliwe na kuapishwa rasmi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mwezi Julai 20, 2020 baada ya ziara yake ya awali Mwezi Julai huko Wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita.