Watu sita wauawa kwa risasi mtwara

Watu
sita wameuawa katika kijiji cha Ngongo Wilaya ya Tandahimba mkoani 
Mtwara na wengine saba kujeruhiwa katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji
baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana Jumanne
Novemba 12, 2019.



Mkurugenzi
wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz amesema Watanzania sita walipigwa
risasi na watu wanaodhaniwa kutoka nchi jirani ya Msumbiji wakati
wakiwa visiwa vya mto Ruvuma wanakofanya shughuli za kilimo.
“Vyombo
vya ulinzi na usalama vitahakikisha wahalifu hao wanapatikana na sheria
kali zitachukuliwa juu yao, niwasihi tu wananchi kuepuka kwenda nchi za
watu bila kuwa na vibali,” amesema.

Kwa
upande wake Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Leberatus
Sabas, amesema kutokana na kazi nzuri wanayoifanya ndio maana wahalifu
wanafanya matukio hayo mipakani.



“Tusikubali hata siku moja wavuke mpaka waje huku ndani tupo bega kwa
mbega na wananchi. Vyombo vyote vya ulinzi na usalama vipo pamoja
tutawasaka, tutawatia mbaroni na hatua kali zitachukuliwa.”