Waziri kamwelwe: afdb endeleeni kufadhili utekelezaji wa miradi ya barabara

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akitoa taarifa ya miradi ya
barabara iliyotekelezwa kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB), wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Amos Cheptoo,
alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akifafanua jambo katika kikao
kilichomkutanisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB) na Wakurugenzi kutoka Sekta ya Ujenzi, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) Amos Cheptoo (kushoto), akisisitiza jambo
katika kikao kilichomkutanisha Mtendaji huyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe pamoja na wakurugenzi kutoka
Sekta ya Ujenzi, jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, (kulia), akimwonesha Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Amos Cheptoo (kushoto),
miradi ya barabara iliyotekelezwa kupitia ufadhili wa Benki hiyo, jijini
Dodoma.
Wakurugenzi kutoka Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), wakimsikiliza Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (hayupo
pichani), katika kikao kilichomkutanisha Waziri huyo na Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, (kushoto), akiwa katika picha ya
pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
Amos Cheptoo, alipofika ofisini kwake na kufanya mazumgumzo nae
kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya barabara inayofadhiliwa na Benki
hiyo, jijini Dodoma.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack
Kamwelwe, ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuendelea
kutekeleza mkakati wake wa ufadhili wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo
ya barabara.

Ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati  Waziri huyo alipokutana
na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo kuhusiana na
maendeleo na  utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara
inayofadhiliwa na benki hiyo.

“Tunawashukuru AfDB kwakuwa
miongoni mwa wadau muhimu katika kutoa ufadhili wa utekelezaji na
uboreshaji wa barabara nyingi nchini, tunaomba muendelee na ufadhili
kwani bado tunahitaji kuendelea kuunganisha mtandao wa barabara kati
yetu na nchi jirani”, amesema Waziri Kamwelwe.
Aidha, Waziri huyo amefafanua kuwa
katika kipindi cha miaka 11 iliyopita Benki hiyo imetoa kiasi cha fedha
zaidi ya shilingi Trilioni mbili (2) kwa ajili ya ujenzi na ukarabati
wa barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 1,655 ambapo kati ya hizo
kilometa 1,168 zimeshakamilika na kilometa 487 bado zinaendelea na
ujenzi wake.
Ametaja baadhi ya miradi ya
barabara iliyofadhiliwa na Benki hiyo  na ambayo imekamilika kwa
kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo ni ukarabati wa barabara ya
Arusha – Namanga (km 105), barabara ya Singida –  Babati – Minjingu ( km
223.5),  barabara ya Iringa – Dodoma (km 260) na barabara ya Namtumbo –
Tunduru (km 193).
Ameongeza kuwa miradi mingine ya
barabara inayoendelea kutekelezwa kupitia ufadhili wa Benki hiyo kuwa ni
ujenzi wa barabara ya Tabora – Koga – Mpanda (km 349), barabara ya
Mabasi Yaendayo Haraka kwa Awamu ya II, barabara ya Tanga – Pangani –
Bagamoyo (km 246), barabara za mzunguko katika jiji la Dodoma, na ujenzi
wa kiwanja cha ndege cha Msalato jijini Dodoma.
Kwa upande wake,  Mkurugenzi
Mtendaji wa AfDB, Amos Cheptoo, amesema kuwa AfDB itaendelea kuunga
mkono na kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara lengo ni
kuifanya Afrika kuendelea kiuchumi.
Amesema kuwa lengo la kuja kwake
Tanzania ni kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na
Benki hiyo ili kuona maendeleo yake.