Waziri mkuu afungua maonesho ya madini geita

Asteria Muhozya na Greyson Mwase, Geita

Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Septemba 22,
2019 amefungua Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya
Madini yaliyoanza tarehe 20 Septemba, 2019 na kutarajiwa kumalizika
tarehe 29 Septemba, 2019.


Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa
pongezi kwa Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa kuboresha shughuli za
madini kupitia kuongeza ajira na vitendea kazi kama vile magari kama
njia mojawapo ya kuboresha ukusanyaji wa maduhuli.

Akielezea
mafanikio ya Soko la Madini Geita tangu kuanzishwa kwake Majaliwa
amesema kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa dhahabu kutoka
takribani kilo 100 hadi kilo 200 na zaidi kwa mwezi na kusisitiza kuwa,
tangu kuanzishwa kwa soko la madini la Geita kiasi cha kilo 1,573
zimezalishwa na kuuzwa.

Katika
hatua nyingine, ameitaka Tume ya Madini kuongeza kasi kwenye ukusanyaji
wa maduhuli ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa
uchumi wa nchi .
 
Aidha,
amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuyatumia vyema
masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini na kuwataka wakuu wa mikoa na
wilaya kuhakikisha yanalindwa.
 
Pia,
amewataka wachimbaji wa madini kutumia tafiti zinazofanywa na Taasisi
ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) kubaini maeneo yanye madini na
kuanza kuchimba ili kuepuka uchimbaji wa kubahatisha.

Amesema
serikali itaendelea kuboresha Sheria na Kanuni ili kuleta tija zaidi na
hivyo kuwataka wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya
madini ikiwemo kutoa taarifa kwenye vyombo vya udhibiti.
 
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wachimbaji wadogo wa
madini kuachana na matumizi ya zebaki na badala yake watumie njia
nyingine mbadala kulingana na miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara
ya Madini pamoja na Tume ya Madini.

Akizungumzia
nafasi ya sekta ya madini katika kuchochea ukuaji wa viwanda, Waziri wa
Madini Doto Biteko amesema kwamba hadi sasa wizara kupitia Tume ya
Madini imekwishatoa leseni mbili za usafishaji wa madini (Refinery
Licence) moja ikiwa mkoani Dodoma na nyingine mkoani Geita

Ameongeza
kuwa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imetoa leseni nne za
uyeyushaji wa madini ya Shaba na Bati ( Smelting Licence )
 
Kuhusu
changamoto ya usafirishaji nje madini ya bati amesema Wizara kwa
kushirikiana na Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) zipo
katika hatua ya mwisho kuwezesha upatikanaji wa Hati ya kusafirisha
madini ya bati nje ya nchi na kuongeza kwamba, hadi kufikia mwezi
Desemba mwaka huu, hati hiyo itakuwa tayari.

Akizungumzia
uanzishwaji wa masoko ya madini, Waziri Biteko amesema masoko hayo
yameleta matokeo chanya huku nidhamu ya watanzania kusimamia masoko na
rasilimali ikiwa imeongezeka hali ambayo imepelekea baadhi ya nchi
zikiwemo za Kongo, Zambia na Msumbiji kutaka kuyatumia masoko ya madini
yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini.

‘’
Wanaotaka kuhujumu masoko waache. Ukifanya hivyo utaambulia vitu viwili
tu, kufilisiwa na kufungwa jela,’’ amesisitiza Waziri Biteko.

Pia,
Waziri Biteko amebainisha kuwa, wadau wa madini nchini hawakatazwi
kuingiza madini nchini kutoka nchi mbalimbali zikiwemo sampuli isipokuwa
tu madini yote yanayopelekwa nje ya nchi ni lazima yazingatie sheria na
taratibu.

Katika
hatua nyingine, Waziri Biteko ameupongeza Mkoa wa Geita kwa kuwa kinara
kwenye usimamizi wa fedha zinazotokana na mpango wa utoaji wa huduma
kwa wananchi wanaozunguka kampuni za madini (CSR) na kuzitaka kuendelea
kufuata sheria na taratibu zinazowekwa na serikali kwenye usimamizi wa
sekta ya madini.

Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema
kuwa, tangu kuanzishwa kwa soko la madini mkoani humo, madini ya dhahabu
yameanza kupatikana kwa wingi na kueleza kwamba kwa mwezi Agosti mwaka
huu jumla ya kilo 504 zimeuzwa sokoni hapo, na kabla ya kuisha kwa mwezi
Septemba tayari kilo 340 zimeuzwa sokoni.

Akizungumzia
lengo la maonesho hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Chacha
Wambura amesema kuwa ni pamoja na kukuza teknolojia ya uchimbaji wa
madini kwa wachimbaji wadogo na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo
katika mkoa wa Geita.

Katika
hatua nyingine ikiwa ni sehemu ya ufunguzi wa maonesho hayo, Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mwongozo wa uwekezaji katika mkoa huo.

Maonesho
hayo yemehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Wakuu wa
Mikoa jirani na Geita, Viongozi wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini,
Wawakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Taasisi
za Kifedha, wadau mbalimbali wa madini na wananchi.

Kaulimbiu
ya maonesho hayo ‘’Madini ni Chachu ya Ukuaji wa uchumi wa Viwanda.
Tuwekeze kwenye Teknolojia bora ya Uzalishaji na Tuyatumie Masoko ya
Madini’