Waziri mkuu asema serikali imeamua kuzuia uingizwaji wa saruji kutoka nje ya nchi ili kulinda viwanda vya ndani

WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa
kushirikiana na wawekezaji katika sekta mbalimbali nchini wakiwemo wenye
viwanda vya kuzalisha saruji.


Amesema
katika kuhakikisha inalinda viwanda vya ndani vya kuzalisha saruji
Serikali imeamua kuzuia uingizwaji wa saruji kutoka nje ya nchi.

Waziri
Mkuu aliyasema hayo leo(Jumanne, Machi 3, 2020) wakati akizungumza na
watumishi wa kiwanda cha saruji cha Simba alipotembelea kiwanda hicho
akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga.

Amesema
licha ya Serikali kupata kodi kutokana na uwepo wa kiwanda hicho, pia
kimesaidia katika kutatua changamoto ya ajira hususani kwa vijana.

Naye,
Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema ameupongeza uongozi wa kiwanda
hicho kwa kuwa wanazingatia sheria zote za madini ukilinganisha na
viwanda vingine.

Awali,
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Reinhardt Swart alisema kiwanda
hicho kinauwezo wa kuzalisha tani milioni 1.25 kwa mwaka lakini kutokana
na mahitaji ya soko kinazalisha tani milioni 1.075 kwa mwaka.

Mkurugenzi
huyo aliongeza kuwa kiwanda hicho kimeajiri jumla ya wafanyakazi 319
kati yao wazawa ni 316 na watumishi watatu ni raia ya kigeni.

Pia,
Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuboresha mazingira ya
uwekezaji nchini.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU