Waziri mkuu: imarisheni mahusiano na wadau

WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mahusiano kati ya Serikali na wadau
mbalimbali wakiwemo viongozi wa kidini, kimila ni muhimu yakaimarishwa.




Ameyasema
hayo jana (Jumanne, Septemba 24, 2019) wakati akipokea taarifa ya mkoa
wa Iringa alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Iringa kwa ajili ya
ziara ya kikazi.




Waziri
Mkuu alisema ni lazima mahusiano hayo yakadumishwa katika ngazi zote
kwa sababu Serikali ipo kwa ajili ya wananchi wote na inawahudumia bila
ya ubaguzi.




Aliwataka
viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia maeneo mbalimbali nchini
wahakikishe wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na uwajibikaji wao uwe na
tija.




 Waziri Mkuu amesisitiza kuwa watendaji wahakikishe suala la ukusanyaji wa mapato linapewa kipaumbele katika maeneo yao.




“Ukusanyaji
wa mapato ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa kwa sababu miradi
ya maendeleo kama ujenzi wa shule haiwezi kutekelezeka bila ya kukusanya
mapato.”




Awali,
Akisoma taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alisema mkoa
huo umepewa zaidi ya sh. bilioni saba kwa ajili ya ujenzi wa hospitali
za wilaya.




Alisema
fedha hizo zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa hospitali kwenye Manispaa
ya Iringa (98%), Halmashauri ya wilaya ya Iringa (90%), Kilolo(99%),
Mufindi (89%).




Mkuu
huyo wa mkoa alisema mbali na fedha hizo za ujenzi wa hospitali pia
Serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi na
ukarabati wa vituo vya afya.




Akizungumzia
kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa, kiongozi huyo alisema wanaendelea
na maandalizi.Mkoa una vijiji 360, mitaa 222 na vitongoji 2,216




(mwisho)


IMETOLEWA NA:


OFISI YA WAZIRI MKUU