Waziri mwakyembe : ukomo wa waandishi wa habari wasiokua na elimu kuanzia diploma ni desemba 2021

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo,Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza na Viongozi wa Mkoa wa
Singida pamoja na wadau wa tasnia ya habari Januari 22,2020 alipokuwa
katika ziara ya kikazi ya kukagua mitambo ya usikivu ya Shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC) iliyoko Mikumbi lengo ikiwa ni kuimarisha
usikivu wa shirika hilo ambao kwa sasa umefikia asilimia zaidi ya 70
nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayoub Ryoba akizungumza Januari 22,2020
wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo
Dkt.Harrison Mwakyembe yenye lengo la kukagua mitambo ya usikivu ya
shirika hilo iliyoko Mikumbi mkoani Singida lengo ikiwa ni kuimarisha
usikivu wa shirika hilo ambapo amesema kwa sasa usikivu umefikia
asilimia zaidi ya 70 nchini.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari –
MAELEZO, Rodney Thadeus akiwasisitiza wanahabari wa mkoa wa Singida
(hawapo pichani) umuhimu wa kuwa na kitambulisho cha Mwanahabari ili
waweze kutekeleza majukumu yao kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria katika
ziara ya kikazi ya Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,
Dkt.Harrison Mwakyembe Mkoani hapo yenye lengo la kukagua mitambo ya
usikivu ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) iliyoko Mikumbi lengo
ikiwa ni kuimarisha usikivu wa shirika hilo ambao kwa sasa umefikia
asilimia zaidi ya 70 nchini pamoja na kukutana na wadau wa tasnia ya
habari mkoani hapo iliyofanyika Januari 22,2020.
Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe pamoja na Naibu wake, Juliana Shonza
wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Rehema Nchimbi
pamoja na viongozi wengine mara baada ya kikao kilichofanyika Januari
22,2020 katika ofisi za mkoa huo kilichokua na lengo la kuzungumzia
ziara ya viongozi hao mkoani hapo.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe akiongozwa na Eng.Upendo Mbele pamoja na
Mkama kukagua mitambo ya usikivu ya Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC) iliyoko Mikumbi Mkoa wa Singida wakati wa ziara yake ya kukagua
mitambo ya Shirika hilo lengo ikiwa ni kuimarisha usikivu ambao kwa sasa
umefikia asilimia zaidi ya 70 nchini iliyofanyika Januari 22,2020.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe pamoja na Naibu wake Juliana Shonza
wakisaini kitabu katika Ofisi ya Mkoa wa Singida walipofika katika ziara
ya kikazi mkoani hapo Januari 22,2020.

Na Shamimu Nyaki –WHUSM, Singida.
WAZIRI wa Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe amesisitiza kuwa itakapofika Desemba
mwaka 2021 ndio mwisho wa waandishi wa habari wasiokua na elimu kuanzia
ngazi ya stashahada kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya
habari ya Mwaka 2016.

Waziri Mwakyembe ametoa kauli hiyo jana
Mkoani Singida alipokuwa anazungumza na wadau wa tasnia ya habari ambapo
amewataka waandishi hao kutambua kuwa kuanzia mwaka 2022 wale ambao
hawatakua na vigezo kulingana na Sheria ya Huduma za Habari hawatakua na
nafasi wala sifa ya kuitwa Waandishi wa Habari.

“Uandishi wa habari ni taaluma kama
taaluma nyingine na sio kimbilio la wale ambao wamefeli katika masomo au
waliokosa kazi ya kufanya,hivyo naomba mtambue kuwa mwaka 2021 ndio
mwisho wa waandishi wasiokua na elimu ya uandishi wa habari kuanzia
ngazi ya stashahada”amesema Mwakyembe.

Aidha Dkt.Mwakyembe amesema kuwa Ibara
ya 18 d ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kuwa kila
mwananchi ana haki ya kupata taarifa sahihi hivyo ni jukumu la
wanahabari kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa ambazo ni sahihi kutoka kwa
watu sahihi na kuzifikisha kwa walengwa kwa usahihi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi
Paskasi Mlagiri ameongeza kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo
wanahabari wasitumike kuchafua watu,kuandika habari za uongo pamoja na
kuepuka kupewa rushwa na watu wanaotaka watumie kalamu zao kuwatafutia
kura na badala yake waandike habari za ukweli ambazo zitalinda amani na
usalama wa nchi yetu.

“Tumeni kalamu zenu vizuri ili msije
kuhatarisha amani ya nchi yetu na pia jiepusheni na kuandika habari kwa
kutegemea kupewa pesa na wale wanaowapa habari ili msije mkaingia katika
mikono ya Sheria” alisema Eng.Mlagiri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa
Idara ya Habari Maelezo, Rodney Thadeus amewataka waandishi wa habari
kuhakikisha kuwa wanakuwa na kitambulisho cha mwanahabari popote
wanapokuwa wanatimiza majukumu yao kwani ndio utambulisho wa tasnia hiyo
huku akieleza kuwa vitambulisho vya wanahabri hao kwa mwaka huu tayari
vinapatikana katika ofisi yake.

Awali,Waziri Mwakyembe alifanya ziara ya
kukagua mitambo ya usikivu wa redio ya Shirika la Utangazaji TBC
iliyopo katika eneo la Mikumbi mkoani hapo ambapo ameeleza kuwa Serikali
inaendelea na juhudi za kuimarisha usikivu wa redio ya Shirika hilo
nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika hilo Dkt.Ayoub Ryoba amesema kuwa mitambo miwili ya Khts 2 kwa
kila mmoja imeshawasili nchini tayari kwa kufungwa ili kuongeza usikivu
katika maeneo mengi nchini ambapo kwa sasa usikivu umefikia asilimia
zaidi ya 70.

“Usikivu wa Shirika la Utangazaji TBC
kwa mwaka 2016 ulikua asilimia 54, mwaka 2019 asilimia 67 na mwaka huu
tunategemea kufikia asilimia zaidi ya 70 lengo ni kufikia watu wengi
zaidi”. Alisema Dkt.Ryoba.

Hata hivyo katika ziara hiyo Waziri
Mwakyembe amepata nafasi ya kupata historia fupi ya wanawake wawili
ambao ni Litti Hema pamoja na litti Kidanka waliopigania uhuru wa kabila
la wanyaturu uliofanywa na Mwalimu Alfred Ringi ambapo imeleeza
ushiriki wa kila mmoja katika kukomboa kabila hilo kwa kutumia mvua na
nyuki ambapo Waziri amemuagiza mwalimu huyo kuendelea kutafuta undani wa
historia hiyo ili
Serikali iweze kuihifadhi.