Wizara ya elimu yakabidhi eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya mfano jijini dodoma

Kaimu Katibu Mkuu Dkt. Ave Maria
Semakafu akizungumza wakati wa kukabidhi eneo litakalojengwa shule ya
Sekondari ya mfano jijini Dodoma.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi
Profesa Evaristo Riwa akifafanua jambo wakati wa makabidhiano ya eneo
litakalojengwa shule ya Sekondari ya mfano jijini Dodoma.
Wataalam kutoka Chuo Kikuu Aridhi,
SUMA JKT na wawakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
wakikagua eneo litakalojengwa shule ya sekondari ya mfano Dodoma
……………..
Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia imekabidhi eneo lenye mita mraba zaidi ya 73,000 lililopo
Iyumbu jijini Dodoma kwa Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) kwa ajili ya
kuanza mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya mfano.
Akizungumza wakati wa makabidhiano
hayo yaliyofanyika jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu Dkt. Ave Maria
Semakafu amesema mradi huo utatekelezwa kwa kutumia Force Account ambapo
Wizara ya Elimu itaunda Kamati itakayosimamia masuala yote yatakayohusu
manunuzi.
“Kwa umuhimu wa mradi huu Wizara
imejipanga kuhakikisha shughuli zote za manunuzi zinafanyika kwa wakati
na vifaa vinavyonunuliwa vinakuwa na ubora ili kuwawezesha SUMA JKT
kutekeleza mradi huu kwa ubora,” amesema Kaimu Katibu Mkuu.
Dkt. Semakafu amefafanua kuwa
pamoja na Wizara kusimamia manunuzi ya mradi huo, Chuo Kikuu cha Ardhi
(ARU) wamepewa jukumu la kusimamia mradi huo ambao ujenzi wake utafanywa
na Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) na kuwataka wahusika wote hawa
kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na ubora.
Aidha, Dkt. Semakafu amewataka
Chuo Kikuu cha Ardhi kuhakikisha wanatoa mahitaji halisi yanayohitajika
katika utekelezaji wa mradi huo kwani kumekuwa na kawaida kwa wataalamu
elekezi kutoa idadi kubwa ya mahitaji na kusababisha kubaki kwa baadhi
ya vifaa ambavyo vimekuwa vikiharibika na kupoteza fedha za umma bure.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Ardhi, Profesa Evaristo Riwa amesema wamejipanga vyema kutekeleza mradi
huo kwa kutoa mahitaji halisi na kuhakikisha unakamilika kwa wakati na
ubora unaotakiwa.
Wakati huo huo Mwakishi wa SUMA
JKT, Captain Deogratias Kaboya amesema wapo tayari kuanza mradi huo na
kuahidi kuukamilisha kwa wakati na ubora huku akisisitiza upatikanaji wa
vifaa kwa wakati.
Ujenzi wa mradi huo unahusisha
ujenzi wa maabara za Fizikia, Kemia, Biolojia, Jiografia, Kompyuta na
Lugha, majengo ya vyoo, majengo ya utawala, madarasa pamoja na mabweni
ya wasichana na wavulana.
Majengo mengine yatakayojengwa
katika mradi huo ni nyumba za walimu, maeneo ya kufulia, bwalo la
chakula pamoja na kutengenezwa maeneo ya michezo na unatarajiwa
kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita.