Na Seif Mangwangi, Arumeru
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umefanikiwa kuhudumia kaya 5,195,605 katika awamu ya pili na tatu ya utekelezaji wa mfuko huo katika halmashauri 186 nchini huku wanawake wakielezwa kuwa wengi zaidi ya wanaume miongoni mwa waliopata huduma kupitia mfuko huo.
Akizungumza jana jijini hapa, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa TASAF Shedrack Mziray amesema katika idadi hiyo ya wanufaikaji, wanawake ni 2,892,643 sawa na asilimia 55.7 na wanaume ni 2,302,962 ambao ni sawa na asilimia 44.3.
Mziray amesema wanufaikaji wakubwa wa mfuko huo wanatoka katika kundi la wanafunzi wenye uhitaji maalum kutoka katika kaya maskini ambao kwa kipindi hicho chote jumla ya wanafunzi Mil 2,139,500 sawa na asilimia 41 wameweza kuhudumiwa.
” Kati ya wanafunzi waliohudumiwa 2,139,500 wanafunzi wanawake walikuwa 1,074,445 na wanaume ni 10,65,055 ambao wote hawa ni wenye umri wa kati ya miaka 6 hadi 18,” amesema.
Aidha Mziray amesema mfuko huo hivi Sasa Uko kwenye tathmini ya utekelezaji wake ili kuweza kubaini wanufaikaji wanaotakiwa kuondolewa baada ya kufanikiwa kupitia ruzuku ambayo wamekuwa wakipata kupitia TASAF.
” Moja ya sera na masharti ya mfuko wa TASAF ni kuwanyanyua wahitaji kutoka hali duni kwenda katika hali ambayo ataweza kujitegemea kiuchumi, hivyo hivi sasa hadi Septemba 2024 tunatarajia kuondoa wanufaikaji 400,000 ambao hali zao za maisha zimeimarika,” amesema.
Kwa upande wake Sara Mshiu ambaye ni Meneja Akiba na kupunguza umaskini wa kaya wa mfuko wa TASAF anasema moja ya changamoto kubwa walizokabiliana nazo ni uwepo wa kaya hewa ambazo hazistahili kupata msaada kupitia mfuko huo.
Hata hivyo amesema baada ya kubaini hilo, mfuko ulitengeneza mfumo dhabiti wa kubaini kaya hizo na umeweza kuziondoa kwa zaidi ya asilimia tisini.
” Changamoto kubwa Ilikuwa ni kuingizwa kwa kaya hewa, na wakati mwingine watendaji wetu walishindwa kuwaondoa kwa kuogopa Hadi uchawi, lakini baada ya kutengenezwa mfumo mzuri, wote waliondolewa,”amesema Sara.
Mfuko wa TASAF ulianzishwa mwaka 2000 nchini ambapo hivi sasa inatekeleza awamu ya tatu ya mradi huo ulioanza mwaka 2020 na kutarajiwa kutamatika Septemba 2025.