Zaidi ya watuhumiwa 100 wa makosa ya uhujumu uchumi waachiwa huru tanzania

Rais wa Tanzania John Magufuli
amesema zaidi ya watu 700 waliokuwa wakishutumiwa kwa makosa ya uhujumu
uchumi, ikiwemo utakatishaji wa fedha , wamekiri kutenda makosa hayo
wakiomba kusamehewa, huku wengine zaidi ya 100 wakiachwa huru.
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli aliwataka waliotuhumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi kukiri na kuomba radhi

Serikali
ya Tanzania awali ilitoa kipindi cha siku saba ili kuandika maombi
hayo, ambapo mwendesha mashtaka mkuu wa serikali alikiri kupokea mamia
ya maombi kutoka kwa watuhumiwa

Rais wa Tanzania, John Pombe
Magufuli alitangaza msamaha Septemba 22, kwa watuhumiwa wa makosa hayo
ambao wataandika barua za kukiri makosa, kuomba radhi na kukubali kulipa
fedha wanazotuhumiwa kujipatia kinyume cha sheria.
Kuachiwa kwa washtakiwa hao kunafungamana na sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai iliyopitishwa septemba mwaka huu inayotoa ruksa ya
kufanyika mapatano baina ya watuhumiwa na mwendesha mashtaka.
Sheria
hiyo inasema kuwa yeyote kati ya mtuhumiwa, wakili wake ama mwendesha
mashtaka anaweza kuanzisha mapatano kwa kuiarifu mahakama.
Katika
makubaliano hayo, mtuhumiwa anaweza kukiri tuhuma ama sehemu ya tuhuma
dhidi yake ili kupata afueni fulani ikiwemo kuondolewa baadhi ya
mashtaka,ama kupunguziwa muda ama aina ya adhabu.

Pamoja na kupokea taarifa ya wale waliokiri makosa yao, kadhalika
Rais Magufuli ametoa muda mwingine wa siku saba kwa washtakiwa wengine
ambao walikuwa bado hawajafikia uamuzi wa kuomba msamaha.
Kwa
mujibu wa sheria za Tanzania, mashtaka ya uhujumu uchumi hayana dhamana,
na wote wanaoshtakiwa kwa makosa hayo husalia rumande mpaka hukumu zao
zinapotolewa.
Tangu aingie madarakani miaka minne iliyopita Rais
Magufuli amekuwa akijipambanua kama kiongozi anayekabiliana na rushwa na
ufisadi. Chini ya utawala wake vigogo kadhaa wameshuhudiwa wakitiwa
korokoroni kwa makosa yanayohusiana na uhujumu uchumi na utakakatishaji
fedha.
 Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Michael Wambura
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Michael Wambura ni moja ya watu maarufu ambao wanakabiliwa na mashtaka
hayo, na Jumatano ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa
amekwishaandika barua kwa DPP kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri
makosa yanayomkabili mahakamani hapo na ameuomba upande wa mashtaka
ufuatilie barua hiyo ili upate majibu kwa haraka.
Wambura ambaye
amefungiwa maisha kujihusisha na soka, alifikishwa mahakamani hapo kwa
mara ya kwanza Februari 11 mwaka huu, akikabiliwa na kesi ya uhujumu
uchumi yenye mashitaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya
shilingi za Tanzania milioni 100.
CHANZO: BBC