Katibu mkuu wa ccm aagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuwashughulikia wadokozi na wezi kwenye miradi

Katibu mkuu wa CCM Dkt.Bashiru Ally akiongea na wananchi wa halmashauri ya Bukoba.
Katibu mkuu wa CCM Dkt.Bashiru Ally akiongea na wananchi wa halmashauri ya Bukoba.

Katibu mkuu wa CCM Dkt.Bashiru Ally akikagua eneo la hospitali ya wilaya ya halmashauri ya Bukoba.

Na Ashura Jumapili -Malunde 1 blog Bukoba.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM )Dkt Bashiru Ally ametoa
maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha wale
waliofanya kazi za ufundi, vibarua, wahudumu na kazi zingine katika
miradi mbalimbali ya serikali wanalipwa kwa wakati hasa kwa miradi
ambayo serikali imetoa fedha hizo.
Bashiru ametoa maagizo hayo leo Desemba 27, 2019 alipotembelea na
kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya halmashauri ya Bukoba ,
ambapo licha ya kuridhishwa na ujenzi huo amedai amekuwa akipokea
malalamiko mbalimbali ya wafanyakazi kutokulipwa kwa wakati licha ya
fedha zote shilingi bilioni 1.5 kufikishwa hospitalini hapo.
Dkt. Bashiru ,alisema wakuu wa mikoa na wilaya wasisite kuwachukulia
hatua kali za kinidhamu na warudishe fedha wasimamizi wa miradi hiyo
ambao wamekula fedha na kushindwa kuwalipa wafanyakazi kwa wakati ili
jasho la wananchi wanyonge lisipotee.
’’Natoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya na mikoa nchi nzima, kuhakikisha
wanalinda miradi hii dhidi ya wadokozi na wezi wa rasilimali hizi za
wananchi, na wale wote waliotoa jasho lao kujenga mradi huu, yaani
mafundi, vibarua, wahudumu na wafanya kazi wengine, walipwe kwa wakati
na jasho la mwananchi lisipotee, kama kuna waliohusika katika
kuchelewesha malipo yao, wachuliwe hatua kali za kinidhanu kwa mujibu wa
sheria za nchi.” Katibu Mkuu amesisitiza.
Aidha, Bashiru alitoa wito kwa wenyeviti wote wa vijiji na mitaa nchi
nzima kutoa ardhi kwa shughuli za jamii ikiwemo ujenzi wa Hospitali,
Shule, Ofisi za umma, na kadhalika kama ambavyo imefanyika katika kijiji
cha Kanazi kwa wananchi kujitolea eneo ambalo ujenzi wa hospitali hiyo
ya halmashuri unaendele, ambapo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza
gharama za ujenzi wa mradi huo.
“Nawashukuru sana wanakijiji cha Kanazi kwa kujitolea eneo hili kwa
ujenzi wa Hospitali hii ya Halmashauri, na ninatoa rai kwa wenyeviti
wote wa aserikali za mitaa na vijiji toeni ardhi kwa matumizi kama haya,
na mfano huu wa kijiji cha Kanazi uigwe nchi nzima’’,alisema.
Ambapo aliongeza kuwa, utaratibu wa kugawa ardhi za vijiji ni lazima uwe
shirikishi na ufanywe na mkutano Mkuu wa kijiji au mtaa na si wajumbe
wa halmshauri ya kijiji pekee ili kupunguza migogoro na kuweka maamuzi
kuwa ya uwazi kwa wananchi wote kama ilivyofanyika kijiji cha Kanazi.
 Dkt Bashiru alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kuiamini
CCM na serikali yake chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, ambapo ameweza
kudhibiti nidhamu katika serikali na Chama, na mafanikio yanayopatikana
sasa ya ujenzi wa Hospitali nchi nzima, vituo vya afya, zahanati,
Barabara, Madaraja, Umeme, miradi ya maji n.k ni matokeo ya jitihada
hizo.
Halmashauri ya wilaya ya Bukoba ni miongozni mwa halmashuri tatu za mkoa
wa Kagera zilizopokea fedha za ujenzi wa hospitali za wilaya, nyingine
ni karagwe na Kyerwa
Awali, Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawilo akimkaribisha
Katibu Mkuu, ameeleza namna serikali ya wilaya, ilivyoridhidhwa na
maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo ambapo licha ya changamoto
mbalimbali ikiwemo hali mvua kwa muda mrefu ujenzi uliendelea na sasa
kufikia hatua ya umaliziaji.