Dk. bashiru atoa msaada wa mbuzi kilo 20 za mchele kwa kituo yatima

Na Baltazar Mashaka , Mwanza 

KATIBU Mkuu wa CCM,  Dk. Bashiru Ally, amekabidhi mbuzi mnyama na kilo 20 za mchele kwa kituo cha Watoto Yatima cha Rahim kilichopo Igelegele, wilayani Nyamagana na kuwashauri watu wanaotaka kuanzisha vituo vya  kulea yatima wawe na mipango ya  miradi endelevu.


Akikabidhi zawadi hiyo kwenye kituo hicho jana kwa niaba ya Dk. Bashiru, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Salum Kalli, alisema watakaoanzisha vituo vya kulea watoto yatima wawe na mipango na wafikirie kubuni na kuanzisha miradi endelevu itakayowasaidia watoto hao kupata mahitaji yao ya kila siku ya kibinadamu badala ya kutegemea misaada ama wafadhili na kuwa ombaomba.

“Tuhakikishe tunakuwa an miradi ama tubuni miradi endelevu badala ya kuwa ombaomba kwani iko siku wafadhili wakigoma hali itakuwa mbaya kwa watoto hawa yatima japo dini inatutaka tuwahudumie wajane na yatima na kama hatuna uwezo, tusilazimishe wakati hatuwezi kuwatimizia mahitaji yao ya elimu, matibabu, malazi na chakula,”alisema.

Katibu huyo wa CCM aliwaasa watoto hao zaidi ya 70 kujituma na kujibidisha kwenye katika masomo yao ya elimu ya dini na mazingira kwa urithi pekee wanaohitaji ni elimu iweze kuwasaidia kwenye maisha yao siku za usoni.

“Dk. Bashiru kaonyesha upendo kwenu na kanituma niwaletee zawadi hii ya kitoweo na mchele. Hivyo mjifunze kwa makini,upendo, mthaminiane, muelekezane kwa mema na kukata  mabaya ili wengine huko nje wajifunze kutoka kwenu.Pia sisi viongozi ujio wetu tutajifunza mengi kutoka kwenu na yawezekana ujio huu ukafungua kheri,”alisema Kalli.

Kwa mujibu wa Kalli, Dk. Bashiru, akiwa kwenye ziara yake wilayani Magu, wananchi wa Kijji cha Ndagalu walimzawadia mbuzi na yeye akaamua kumtoa mbuzi huyo na kilo 20 za mchele kwa kituo hicho cha yatima.

Awali Imamu wa Msikiti unaolea watoto hao,Ramadhani Juma alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo cha vitanda na magodoro, vifaa vya kujifunzia vya elimu ya dini na mazingira (vitendea kazi), vyumba vitatu vya madarasa  (madrasa),fedha za chakula na matibabu, na ada kwa wanaojiunga na masomo ya sekondari.
Alisema changmoto nyingine ni posho ya mwalimu wa madrasa ambapo ili kukidhi mahitaji ya watoto hao wanachangishana na wakati mwingine kuomba misaada kwa watu mbalimbali ambayo pia haikidhi  mahitaji.