|
Mkurugenzi wa FCS Francis Kiwanga akihojiwa na Waandishi wa Habari |
Na Seif Mangwangi, Arusha
JAMII imetakiwa kuwa tayari kujifunza na kukubaliana na mabadiliko ya teknolojia ili kukuza uchumi na kujipatia kipato cha kutosha na chenye uhakika.
Wito huo umetolewa na Mwakilishi na mfanyakazi wa shirika la Apple Inc kutoka nchini Marekani, Mtanzania, Aboubakar Ally katika ufunguzi wa Wiki ya Azaki iliyoanza Jana Jijini Arusha.
Amesema mabadiliko ya kiteknolojia ya kidigital duniani kwa sasa yamekua yakiendelea kukua kwa kasi kubwa na kuleta matokeo mazuri hivyo jamii iwe tayari kuyapokea na kupenda kutumia Teknolojia hizo.
Aboubakar ambaye ni miongoni mwa Watanzania wachache wabobezi kwenye Teknolojia amesema kwa kutumia Teknolojia yeye na wenzake wameweza kuanzisha shamba la hekari 20 la mbogamboga katika mji wa Boston ambapo wameweza kuanzisha nishati ya umeme kwa kutumia gesi kutokana na mji huo kuwa na baridi kali na pia kuwasaidia kuongeza hewa ya oxygen ili waweze kupata mazao Bora.
“Teknolojia imetusaidia kuanzisha hili shamba kwenye eneo ambalo haliwezi kulimwa kutokana na Hali yake ya hewa, wakati bado tunaendelea kumalizia ujenzi tayari tumeshapata wateja wa mazao yetu na kwa mwaka tu tutakuwa tunaingiza faida ya Dola milioni7,”amesema.
Mkurugenzi wa Muungano wa Asasi za Kiraia (FCS), Francis Kiwanga amesema kutokana na Kasi ya mabadiliko yaliyopo katika Sayansi na Teknolojia ni lazima watanzania wabadilike na kuendana na kasi hiyo Ili Kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji huduma ikiwa ni pamoja na kujua aina Bora ya Teknolojia ya kuendana nayo na kujiepusha na athari zake.
“Mabadiliko ya teknolojia yanakuwa Kwa kasi Sana lakini vijana wanapaswa kuangalia namna Bora yakuweza kuya akisi bila kuathiri Jamii na ndio maana tunakuwa na mijadala kama hii kuchagua ni teknolojia Gani inafaa na ipi haifai” Amesema Kiwanga.
Kwa upande wake Mrajisi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Zanzibar Ahmed Abdulah ametoa rai kwa Asasi za kiraia kuwa mstari wa mbele katika kubeba maono ya Jamii Kwa kuwa na matumizi Bora ya Teknolojia.
“Ni jukumu letu kama Asasi kuona Jamii inachagua matumizi sahihi ya teknolojia na siyo kivingine, Matumizi yanapokuwa sahihi yanaleta mtazamo chanya kwenye Jamii”amesema
Naye Mwakilishi wa Meya wa Jiji la Arusha Isaya Doita amewataka vijana nchini kuhakikisha wanakuwa na matumizi yenye tija katika mitandao ya kijamii Kwa lengo la kujiingizia kipato Kwa namna iliyohalali.
Amewataka pia kujitahidi kujifunza namna Bora ya kuendana na Teknolojia hususani katika mitandao ya kijamii huku wakiiga mifano ya waliofanikiwa kupitia mitandao hiyo na kuahidi kuwa kama Serikali wanaendelea kutoa wito kwa vijana kufanya Mabadiliko chanya kupitia teknolojia.
Abubakari Ally ni miongoni mwa vijana waliofanikiwa kupitia teknolojia ambapo ameweza kubuni na kuendeleza mradi wa Kilimo Cha kidijitali kupitia teknolojia huku akisema ana uhakika wa kupata zaidi ya dola milioni 20 Kwa heka 22 alizowekeza katika Kilimo.
Tanzania imeendelea kushuka Kasi kufuatana na mabadiliko ya kiteknolojia,Ili kuwa na mifumo Bora yenye kurahisha utoaji huduma.
PICHA MBALIMBALI ZA MATUKIO