Daladala walalamika kushuka biashara baada ya corona

 

Na
Mwandishi Wetu, 
Arusha.

Madereva wa mabasi madogo ya abiria maarufu kama
daladala wamelalamikia kushuka kwa biashara hiyo mara baada ya kuzuka kwa
ugonjwa wa mlipuko wa homa kali ya mapafu COVID-19.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti madereva hao wamesema
kutokana na agizo la kuepuka msongamano ili kuthibiti kuenea kwa ugonjwa huo,
wamelezimika kubeba abiria wachache tofauti na kipindi cha nyuma.

“Sasa hivi ni mwendo wa level seat (akimaanisha
hakuna kusimamisha abiria ndani ya gari), hatua hii imeshusha makusanyo yetu ya
kila siku kwa sababu abiria waliokuwa wakisimama walikuwa wanaongeza hesabu”
Alisema Babuu Msemo dereva wa daladala kituo cha Kilombero.

Kauli hiyo iliungwa mkono na dereva mwenzake
anayefanya safari za mjini-Njiro Salim Njoya ambaye alisema licha ya kubeba
abiria kwa idadi ya viti vya gari lakini pia hawaruhusiwi kubeba abiria wa
njiani kwani kila anayepanda anapaswa kunawa mikono.

“Unajua hili la kunawa mikono nalo limeleta shida,
kwa sababu hata ukitaka kupakiza abiria wa njiani, wale waliopo ndani ya gari
wanaanza kupiga kelele wakisema hajanawa mikono, na sisi hatutembei na maji
kwenye gari, na hata ukiwa nayo ni kupoteza tu muda kuanza kuwanawisha njiani”
Alisema Njoya

Walisema licha ya kuwa serikali ina nia njema ya
kutaka kukabiliana na janga hilo lakini isingepiga marufuku kusimamisha abiria
badala yake wangeweka utaratibu wa kila abiria kuvaa barakoa, na kunawa kabla
ya kupanda ili kuinusuru biashara yao.

Kwa upande wa abiria wamefurahishwa na kitendo hicho
kwani wamesema kwa sasa wanasafiri kwa uhuru na amani zaidi tofauti na kipindi
cha nyuma ambapo walikuwa wanajazwa kupita kiasi hali inayopelekea hewa kuwa
nzito ndani ya gari.

“Wakati mwingine tunasafiri na wagonjwa au watoto
wadogo, sasa ukikutana na daladala uliyojaza kupita kiasi ni changamoto, kama
ni mtoto utashangaa anaanza kulia, na kama ni mgonjwa anazidishiwa tatizo’
Alisema Mama Aron.

Msimamizi wa kituo hicho cha daladala Joshua Lemomo
amesema wamepokea maelekezo kutoka kwa wataalamu afya kuhakiklisha hakuna daladala
itakayotoka standi ikiwa imebeba abiria zaidi ya idadi ya viti vilivyopo na
kwamba wataendelea kusimamia agizo hilo.